Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu Thinking, Fast and Slow kilichoandikwa na mwanasaikolojia Daniel Kahneman.

Hiki ni kitabu kinachotuonesha mifumo miwili ya kufikiri iliyopo kwenye akili zetu, jinsi inavyofanya maamuzi na ukomo wake katika maamuzi tunayoyafikia. Mifumo hii ni ya kufikirika, lakini matokeo yake yako wazi kwenye maisha yetu ya kila siku.

thinking fast and slow.jpg

Mfumo wa kwanza huwa unafanya maamuzi kwa haraka, kwa kutumia hisia na bila hata ya kufikiri kwa kina. Mfumo huu unatumia mazoea ambayo tayari yamejengeka ndani ya mtu kufikia maamuzi, hata kabla mtu hajafikiria kitu kwa kina.

Mfumo wa pili huwa unafanya maamuzi taratibu, kwa kufikiria kwa kina na kuwa na vigezo na ushahidi wa kufikia maamuzi hayo. Mfumo huu unahitaji nguvu nyingi na pia huchoka haraka, kwa sababu zoezi la kufikiri siyo rahisi.

Kwenye kitabu mwandishi anatuonesha jinsi maamuzi tunayoyafanya yanavyohusisha mifumo hiyo, maamuzi mengi yakifanywa na mfumo wa kwanza, lakini mara nyingi maamuzi hayo huwa siyo sahihi.

Pia tutajifunza jinsi ambavyo udhaifu wa mfumo wa kwanza wa kufikiri unavyotumiwa na watu mbalimbali, hasa wale wanaotaka kuwashawishi wengine kufanya vitu fulani. Kwa kujua udhaifu wa mfumo huo wa kwanza, unaweza kuwashawishi wengine kufanya kile unachotaka.

Kuhusu Mwandishi.

Daniel Kahneman (kuzaliwa Machi 5, 1934) ni mwanasaikolojia na mchumi wa nchini Israel ambaye kazi zake saikolojia zimekuwa na mchango mkubwa kwenye ufanyaji wa maamuzi, tabia na uchumi pia.

Mwaka 2002 Daniel alipewa tuzo ya Nobel kwenye uchumi kutokana na mchango wake kwenye saikolojia ya kufanya maamuzi kiuchumi.

Daniel kwa kushirikiana na wanasaikolojia wengine kama Amos Tversky amefanya tafiti nyingi na kuandika vitabu mbalimbali kwenye eneo la saikolojia na maamuzi.

Kupitia tafiti hizi, Daniel amegundua kwamba watu huwa wanafanya maamuzi kwa hisia na siyo kufikiria. Pia amegundua udhaifu uliopo kwenye mchakato wa ufanyaji maamuzi, ambapo kuna njia za mkato huwa tunazitumia kufikia maamuzi.

Kwenye kitabu chake cha Thinking, Fast and Slow ameshirikisha yale yote aliyojifunza na kugundua kupitia tafiti mbalimbali kuhusu saikolojia ya mwanadamu hasa kwenye upande wa kufikiri na kufanya maamuzi.

Daniel ni profesa wa saikolojia kwenye chuo kikuu cha Princeton na pia mwanzilishi wa kampuni ya TGG Group ambayo inatoa ushauri elekezi kwenye biashara na utoaji wa misaada.

Utangulizi Kutoka Kwa Mwandishi.

Ukiulizwa unafikiria nini, unaweza kujibu kwa urahisi. Unaamini unajua kile kinachoendelea kwenye akili yako, ambapo kuna mawazo mbalimbali yanayofuatana. Lakini hivyo sivyo akili yako inavyofanya kazi pekee. Mawazo mengi unayokuwa kwenye akili yako, huwa yanaibuka hata bila ya wewe kujua yamefikaje kwenye akili yako. Mawazo hayo huwa yanatengenezwa yenyewe kutokana na kile kinachoendelea kwenye mazingira yako. Kwa mfano umekaa mahali, ukaondoka na baada tu ya kuondoka kikatokea kitu ambacho ni hatari. Hapo akili yako inakuwa imeshaiona hatari kabla hata ya wewe kuweza kufikiria uwepo wa hatari hiyo.

Hata wakati ambao hufikirii, akili yako inaendelea kufanya kazi kimya kimya na kuzalisha hisia, nadharia na maamuzi mbalimbali kulingana na kile kinachoendelea ndani na nje ya mwili wako.

Kwenye kitabu hiki utakwenda kujifunza udhaifu uliopo kwenye akili zetu katika kufikia maamuzi yake. Kwa kujua udhaifu huo haimaanishi kwamba akili zetu haziwezi kuwa vizuri. Bali inatufundisha jinsi ya kuepuka madhaifu hayo, hasa pale unapofanya maamuzi magumu. Lakini zaidi inatusaidia kujua nyakati au mazingira ambayo udhaifu huo unaweza kutumika vibaya kwetu.

Huwa tuna tabia ya kufanya maamuzi kwa hisia badala ya kufikiri, tunaamini zaidi kile kinachoonekana kuliko kisichoonekana na pia huwa tunang’ang’ana na kile tunachokiamini hata kama siyo sahihi. Hayo ndiyo yamekuwa chanzo cha kufanya maamuzi yasiyo sahihi na wakati mwingine kutapeliwa.

Wanasayansi wa miaka ya 1970 walikubali vitu viwili kuhusu asili ya binadamu. Moja watu huwa wanafanya maamuzi kwa fikra na mwazo yao ni mazuri. Mbili hisia kama za hofu, chuki na nyinginezo zinakuja pale mtu anapoacha kufikiri. Kupitia tafiti na kitabu hiki utajifunza vitu hivyo viwili siyo sahihi. Watu hawafanyi maamuzi kwa kufikiri mara zote na makosa ya maamuzi wanayofanya watu hayatokani na hisia, bali jinsi mfumo wa kufikiri ulivyo. Kuna udhaifu upo kwenye mfumo wa kufikiri ambao usipozingatiwa makosa yanafanyika.

Udhaifu mkubwa kwenye kufikiri unatokana na kuwepo kwa njia za mkato (heuristics) na upendeleo (biases) kwenye maamuzi tunayoyafanya. Hivyo unafikia maamuzi siyo kwa sababu ndiyo sahihi, bali kwa sababu ni rahisi (kutokana na urahisi wa kuyafikia) au yanaendana na kile unachoamini au kukubaliana nacho (kutokana na upendeleo).

Kwa kujua udhaifu huo na kuuzingatia, inasaidia kufanya maamuzi bora na sahihi kwenye kila eneo la kazi, biashara na maisha kwa ujumla.

Mfano wa udhaifu tulionao ni kuamini kile tunachosikia zaidi ndiyo muhimu zaidi. Mfano vyombo vya habari vinapoongelea jambo fulani muda mwingi, basi tunalichukulia lina uzito mkubwa. Kumbe halina uzito, ila tunafikiria hivyo kwa sababu tumesikia sana. Mfano mzuri ni ugaidi, huwa unapewa uzito kwa sababu unaongelewa sana. Lakini ukiangalia takwimu, kuna watu wengi wanaojiua wenyewe au kufa kwa ajali kuliko wanaokufa kwa matendo ya kigaidi.

Kitabu hiki pia kitakuonesha nafasi ya bahati kwenye mafanikio yoyote yale. Pamoja na juhudi ambazo watu wanakuwa wameweka, kuna mambo nje ya uwezo wao yanakuwa yametokea na kusaidia, ambapo kama yasingetokea wasingepata mafanikio waliyopata.

Kitabu hiki kinakwenda kukusaidia kujua jinsi akili yako inavyofanya kazi, kupitia tafiti mbalimbali za kisaikolojia. Utaona jinsi unavyoangukia kwenye kufanya maamuzi yasiyo sahihi kutokana na udhaifu uliopo kwenye mifumo yetu ya kufikiri.

Kila unachofanya kwenye maisha yako, akili yako huwa inakihifadhi, kila kinachotokea kwenye mazingira, akili hiyo inahifadhi na baadaye kutumia kwenye kufanya maamuzi. Hii ndiyo inayofanya waliobobea kwenye eneo fulani kuweza kufanya maamuzi ya haraka kuliko ambao hawajabobea. Kwa sababu hao waliobobea wana kumbukumbu nyingi kwenye akili zao ambapo inasaidia kufikia maamuzi haraka. Mfano daktari ambaye ni mzoefu, anaweza kumwangalia mgonjwa mara moja na akajua ana shida gani, au kusikiliza maelezo yake na akajua shida yake. Hiyo ni kwa sababu ameshaona wagonjwa wengi na kusikia maelezo mengi na hivyo akili yake imetunza yote hayo.

Lakini kutokana na udhaifu uliopo kwenye mfumo wetu wa kufikiri, hata mazoea hayo kuna wakati yanaweza kutumika vibaya, hasa pale kunapokuwa na mabadiliko madogo kwenye kile ambacho mtu amezoea. Pale ambapo mambo hayajajipanga kama tulivyozoea, akili huwa ina tabia ya kutengeneza kile ilichozoea na hapo kupelekea mtu kufanya maamuzi ambayo siyo sahihi.

Kwenye kitabu hiki tunakwenda kujifunza mfumo wa kufikiri na kufanya maamuzi wa akili zetu ambao umegawanyika kwenye sehemu mbili, moja inafikiri haraka na nyingine taratibu. Maamuzi mengi yamekuwa yanafanya na mfumo wa kwanza ambao ni wa haraka, lakini pia una madhaifu yake. Huku mfumo wa pili ukiwa wa taratibu na unaorekebisha mfumo wa kwanza.

Kupata uchambuzi wa kina wa kitabu hiki cha Thinking, Fast and Slow jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.