Umeamka asubuhi, unataka kuwahi mahali, unajua kabisa usafiri wako uko vizuri, ila asubuhi hiyo unajaribu kuuwasha na hauwaki. Ulishapanga kabisa muda uliozoea kufika eneo husika na sasa usafiri ambao umekuwa unatumia kila siku hauwaki. Unaweza kupata hasira, ukakazana kuendelea kuwasha ukitegemea uwake kwa haraka kama ulivyo na haraka wewe, lakini hilo halitasaidia.

Kuna ujumbe muhimu wa barua pepe unaopaswa kuutuma kwa haraka, lakini mtandao wa intaneti uko chini sana, muda unakwenda na mtandao haufungui hata barua pepe. Unapatwa hasira na kutaka hata kupiga kifaa chako, lakini hasira hizo haziwezi kuufanya mtandao uwe na kasi.

Hasira hazijawahi kuwa na manufaa kwenye jambo lolote lile, lakini ni ajabu zaidi kutegemea hasira zako kubadili kanuni za asili.

Dunia huwa inajiendesha kwa kanuni zake za asili, ambazo haziangalii matakwa ya mtu mmoja mmoja. Hivyo kama unataka kuwa na maisha tulivu, mara zote angalia kanuni za asili na zifuate hizo.

Kama kuna kitu ambacho hakifanyi kazi kwa namna ulivyozoea au kutegemea kifanye kazi, kuna kisababisho, wewe kulazimisha kifanye kazi hakutaondoa kile kisababisho.

Ni wajibu wako kuelewa nini kinachosababisha, kisha kukishughulikia ili uweze kuendelea na kile unachotaka kufanya. Ukisharuhusu hasira zikuingie, ndiyo kabisa akili yako itagoma kuona kisababisho na hivyo utazidi kuwa kwenye mkwamo.

Hii ni kwa mambo yote unayojihusisha nayo, kama hupati matokeo unayopata, hasira hazitasaidia, bali angalia kile kinachoingia na tafuta kinachozuia matokeo yasiwe kama unavyotaka yawe. Ni kanuni, siyo kubahatisha au ushirikina.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha