“You should accept yourself, not as a master, but as a ser vant, and then all your bad feelings, your anxiety, alarm, uncertainty, and dissatisfaction will be changed into calm ness and peace. You will be filled inside with a clear vision of your purpose, and with a great joy.” – Leo Tolstoy

Jikubali kama mhudumu, kisha wahudumie wengine.
Chochote unachofanya usijiangalie unapata nini,
Bali angalia unawanufaishaje wengine, unakuwaje wa huduma kwa wengine.

Wasiwasi, hofu, kujisikia vibaya, kukosa uhakika yote ni matokeo ya kujiangalia wewe zaidi.
Dawa ya haya ni kuacha kujiangalia wewe tu na kuwaangalia wengine pia.

Unapoweka mkazo kwenye kuwahudumia wengine, matatizo yako binafsi hayapati nafasi ya kukusumbua.
Lakini unapojiangalia wewe tu, utaona kila aina ya matatizo na magumu.

Unapaswa kujisahau mwenyewe kwa kuwahudumia wengine.
Unapaswa kujaza maono yako makubwa kwenye fikra zako, ukiangalia ni namna gani unatoa huduma bora kwa wengine.

Kwa bahati mbaya sana, zama hizi, kila mtu anataka ahudumiwe na siyo kuhudumu.
Kila mtu anataka asikilizwe na siyo kusikiliza.
Kila mtu anataka awe na wafuasi na siyo yeye kuwa mfuasi.
Hakuna ubaya kwenye vitu hivyo, ila vinakuwa changamoto pale kila mtu anapovifanya.

Angalia mitandao ya kijamii,
Kila mtu anapiga kelele,
Kila mtu anatafuta wafuasi wengi zaidi,
Halafu mwisho wa siku anapata nini?
Achana na mbio hizo zisizo na tija na kuwa mtu wa kuhudumu.
Chagua watu utakaowahudumia vizuri, peleka nguvu zako kwao na utapata matokeo bora zaidi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu hasira haziwezi kubadili kanunu za asili, soma hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/09/18/2088

Pia niliandika ukurasa kuhusu kauli ya kishujaa na inayokupa uhuru, nikaomba kila mmoja aweke maoni ni kauli ipi anajiambia, hii ni sehemu nzuri ya kuchagua unahudumu kwenye nini. Kama hukuweka maoni yako, tafadhali fanya hivyo sasa, fungua hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/09/16/2086

Na kama ambavyo nimewahi kukuambia, kazi yangu ni wewe, nimejitoa kukuhudumia kwa kukuandalia na kukupa maarifa sahihi na mwongozo wa kukuwezesha kufika kwenye mafanikio makubwa. Ninachojua na kuamini ni mafanikio yako ndiyo mafanikio yangu, hivyo nasumbuka zaidi na wewe, nikijua unavyofanikiwa zaidi, ndivyo na mimi nafanikiwa zaidi.
Hivyo niombe ujitume sana kwa namna unavyojifunza na karibu tuendelee kuwa pamoja.

Rafiki yako,
Kocha Dr Makirita Amani.