Moja ya vikwazo ambavyo vimekuwa vinawazuia watu kufanikiwa lakini hawavijui ni umri. Wengi hawajawahi kukaa chini na kutafakari jinsi umri unaathiri hatua wanazochukua, wanadhani wanachofanya ndiyo wanachotaka, kumbe umri wao umekuwa na ushawishi.
Kwa vijana, wengi huwa hawaridhiki na kile walichonacho, wanapenda mabadiliko ya haraka, wapo tayari kujaribu vitu vipya na hawapendi kufanya kitu cha kujirudia rudia. Kwa hali hii, wanajaribu mambo mengi mapya, lakini wengi hawadumu na chochote wanachojaribu mpaka kufikia mafanikio.
Kwa wazee, huwa wanaridhika na kile walichonacho, hawapendi mabadiliko ya haraka na hawapo tayari kujaribu vitu vipya na wakishapata njia inayofanya kazi, basi hurudia hiyo mara zote. Kwa hali hii, wanakuwa na msimamo kwenye yale wanayofanya lakini kwa kutokujaribu vitu vipya wanashindwa kufanya makubwa zaidi.
Hivyo chukua tahadhari;
Unapokuwa kijana, endelea na hali ya kujaribu vitu vipya, lakini jipe muda wa kuvifanyia kazi mpaka upate matokeo makubwa, usitegemee matokeo ya haraka. Chagua kile ambacho utakifanya kwa maisha yako yote, kisha kila mara angalia namna ya kukiboresha. Ukishajua unachotaka kufanyia kazi, acha kupoteza muda kwenye kujaribu vitu vipya kwenye maeneo mengine na kupenda kwako mabadiliko kutumie kuboresha kile unachofanya. Pia jiwekee utaratibu wa jinsi unavyofanya mambo yako na kuutumia huo, itakupunguzia changamoto mbalimbali kama hali ya kuahirisha mambo.
Unapokuwa mzee, endelea na msimamo wako kwenye kile ambacho umechagua kufanyia kazi, lakini kuwa tayari kujaribu vitu vipya, vya kuboresha zaidi kile unachofanya. Kila mara tafakari na jiulize ni kwa namna gani unaweza kufanya kwa ubora zaidi kile unachofanya sasa. Usihofie mabadiliko kwa kuona kuna vitu huvijui kwa umri wako, badala yake kila wakati jifunze. Kadiri unavyojifunza utaona njia bora za kufanya kile unachofanya.
Jinsi umri wako unachukulia mambo unaweza kuwa kikwazo, kama hujui jinsi hilo lilivyo kikwazo. Ukishajua, unageuza kikwazo hicho kuwa faida ambayo itakunufaisha zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante kocha kwa makala hii.
LikeLike