Mpendwa rafiki yangu,
Wewe mzazi ni wawakili wa mtoto wako hapa duniani. Umepewa mamlaka ya kubariki na kulaani lakini usitumie mdomo wako kulaani mtoto wako bali tumia mdomo wako kubariki, kuo mtoto wako.
Umepewa jukumu la kuchunga watoto wako. Pale unapaswa kuwalisha, kuonya, kukemea na hata kukaripia pale unapoona mwenendo wa mtoto siyo.
Wakati mwingine unakuwa una hasira unajikuta umemtamkia mtoto maneno ya ajabu na hata kumtukana na kumporomoshea matusi mengi.
Lakini watoto huwa wanakaa kimya lakini matusi na yale maneno huwa yanawaingia akili na baadaye yakuja kuwaathiri.
Kuwa makini na kichwa chako maana kinaumba siyo hadithi ya kutunga bali ni ukweli, hebu leo anza kumnenea mtoto x maneno mazuri kila siku anapoamka na mtoto y maneno hasi uone kama mtoto y atakuwa salama.
Njia rahisi ya kumpoteza mtoto ni pale mzazi unapokuwa unaonesha upendeleo wa wazi kwa watoto ulio nao. Badala ya kujenga utakuwa unabomoa na kusababisha mpasuko katika familia yako.
Wazazi wanachangia kumfanya mtoto kuwa bora au kuwa hovyo kadiri ya malezi unayompatia mtoto wako. Atakua bora kama wazazi wanashikiriki katika kumlea vema.
Nimejifunza katika familia nyingi wazazi wengi hawawafundishi watoto wao mambo ya kiimani. Familia nyingi zimekumbatia usasa kuliko mambo ya kiimani. Watoto hawafundishwi misingi ya kiimani kadiri ya dini zao.
Watoto wengi hawana misingi ya kiimani, hawafundishwi kumjua Mungu bali wazazi wanakazania mambo ya ulimwengu.
Ukimfundisha mtoto wako vizuri misingi ya imani yako atakua na maadili mazuri. Kwa sababu kila dini ina mafundisho mazuri juu watoto hivyo yatumie kumfundisha mtoto wako ili awe vizuri.
Wazazi wanawaacha watoto wakitangatanga kiimani bila usaidizi. Wazazi msipojenga misingi bora ya watoto tutajenga taila la hovyo.
Wazazi wafundisheni watoto kusema, asante, karibu, kuomba samahani na kutambua kosa lao na siyo kuficha kosa. Kwa mfano, wako watoto wadogo ambao huwa wanafanya makosa lakini baadhi ya wazazi wanaficha kosa la mtoto, unakuta mtoto akifanya kosa badala aachwe ajifunze kosa lake tena wazazi wanamwambia tema mate tumchape ni huu ukuta ndiyo umesababisha.
Mtoto anapokosea, usimfiche mweleze ukweli na atambue kosa alilofanya. Kwa mfano, mtoto anaweza kuambiwa zima Tv uende ukale au ukasome lakini mtoto atahisi ameonewa kwa kitendo cha kuambiwa kuzima tv na kuanza kulia, anapolia mwache alie atambue kuwa kuna vitu vyenye maana na sivyo na maana na siyo kutetea ujinga.
Mzazi ni mwalimu wa kwanza katika malezi ya mtoto hivyo wajibika ili mtoto wako awe vizuri ni jukumu lako na wala siyo la mtu mwingine.
Usipomfundisha mtoto wako leo dunia itakuja kukusaidia kukufundishia mtoto wako bila huruma kwa adhabu na riba juu unayoikwepa kulipa leo.
Unaposhindwa kumlea mtoto waki vizuri atakua mzigo kwako na kwa jamii nzima. Wajibika katika malezi ya watoto wako ipasavyo ili kuepuka kuwa tatizo katika jamii.
Hatua ya kuchukua leo; wewe kama mzazi hakikisha unajitoa bila kujibakiza katika malezi ya mtoto wako.
Nenda kamfundishe mtoto imani thabiti na kumjua Mungu na siyo kumfundisha mtoto chuki bali upendo.
Simamia wajibu uliopewa kama mzazi ukiwaacha watoto wapotee damu yao itakulilia maana wewe kama mzazi umeshindwa kutimiza wajibu wako.
Mwisho, mtoto ni malezi. Na wahenga wanasema mkunje samaki angali mbichi hivyo na wewe anza kumfundisha mtoto wakati akiwa bado mdogo na kile unachomfundisha na wewe uwe unakiishi kwa mfano kama unamwambia mtoto aende nyumba za ibada hakikisha na wewe unaenda. Fundisha kwa matendo na siyo maneno.
Makala hii imeandikwa na
Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali.
Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa
http://kessydeo.home.blog ,vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI. Karibu sana.
Ukawe na siku bora sana rafiki.
Rafiki na mwalimu wako,
Mwl, Deogratius kessy
0717101505//0767101504
deokessy.dk@gmail.com //
Asante sana