Kinachotufanya tuahirishe yale tunayopanga kufanya, ni kwa sababu tuna machaguo mengi ya nini tunaweza kufanya na muda tulionao.

Hivyo kile tulichopanga kufanya kinapoonekana kigumu au chenye changamoto, ni rahisi kukimbilia kwenye kingine kinachoonekana rahisi zaidi.

Kwa njia hii, unajikuta ukitoroka yale uliyopanga kufanya, ukijipa sababu nyingi unazoweza kuona ni za kweli, lakini unakuwa unajidanganya.

Njia bora ya kuondokana na hali hii ya kutoroka, ni kujiwekea ukomo wa jinsi unavyoweza kutumia muda uliotenga.

Mfano kama umetenga muda fulani kwa ajili ya kufanya kitu ambacho ni muhimu, basi jiwekee ukomo kwamba utafanya kitu hicho au kingine usichokipenda. Na hapo usijiruhusu kufanya kingine tofauti na vitu hivyo viwili.

Kama umejiambia kuanzia saa moja mpaka saa mbili utaandika, unapofika muda huo, jiambie unaweza kufanya moja kati ya mawili, kuandika au kufanya kingine usichopenda (hapa chagua kile ambacho hupendi kweli kukifanya, unaweza hata kuchagua kuhesabu namba mpaka muda huo unaisha).

Unapojiwekea ukomo huu, unasukumwa kufanya kile ulichopanga, kwa sababu mbadala wake siyo tu utakuchosha, bali pia hautakuwa na manufaa yoyote kwako.

Huwa tunatoroka kufanya kitu, pale tunapokuwa na mbadala ambao tunaufurahia zaidi. Mfano umepanga kuandika, lakini kuandika ni kugumu, hivyo unakimbilia kwenye mitandao ya kijamii, ambayo ni rahisi na inakupa raha ya muda mfupi.

Unapojiwekea ukomo wa jinsi unatumia muda wako, huku kile ulichopanga kufanya kikiwa ndiyo chenye manufaa ukilinganisha na mbadala wake, utasukumwa kufanya kilicho sahihi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha