Kuna wakati unaweza kuona watu wanahangaika na kitu kisichokuwa sahihi, na unajua kabisa siyo sahihi lakini unaona kikiendelea tu, hakikatazwi na wala wanaofanya hawakamatwi.
Kwa vile kitu hicho kinaendelea, watu wananufaika kweli kweli, na wanakuonesha wazi kwamba kitu hicho kinawanufaisha.
Mwanzo ulikuwa na msimamo kwamba hutajihusisha na kitu hicho, kwa sababu siyo sahihi, lakini siku zinaenda, watu wanaojihusisha wanafanikiwa.
Unaona wewe ndiye ambaye hauko sahihi, unaamua na wewe ushiriki, ili na wewe unufaike. Unashiriki na muda siyo mrefu kitu hicho kinakatazwa kwa sababu siyo sahihi, umeweka rasilimali zako na zinaishia kupotea.
Hapa ndipo wengi hulalamikia mamlaka zinazohusika, wengi hulaumu kwa nini hazikukataza kitu hicho mapema, kwa nini zilisubiri mpaka watu wamewekeza rasilimali zao (mali, muda, fedha) ndiyo wakikataze huku wakiwasababishia hasara?
Ninachotaka kukuambia hapa rafiki yangu ni hiki, unapojikuta kwenye hali kama hiyo, huna wa kumlaumu bali ujinga, uzembe na tamaa zako mwenyewe. Njia sahihi za kufanikiwa zipo, lakini unaenda kutafuta za mkato kwa sababu una haraka na hutaki kuweka kazi. Mwanzo ulikuwa na wasiwasi kwamba kitu hicho siyo sahihi, kwa sababu kuna misingi uliona haipo sawa, ila kwa kuwa wengi wanafanya na wananufaika, unaenda kinyume na msimamo wako.
Iko hivi rafiki, kitu chochote ambacho siyo sahihi, huwa kinapata umaarufu wa kasi na wa haraka, watu hunufaika kweli mwanzoni, lakini baadaye huja kuwa maumivu. Hivyo kama umekagua kitu kwa vigezo ulivyonavyo na kikawa siyo sahihi, usiangalie wengine wananufaikaje, bali baki kwenye msimamo kwako kwamba siyo kitu sahihi.
Jambo la pili muhimu sana kuelewa ambalo litakusaidia kwenye maisha ni hili, uongo huwa unabaki kuwa uongo hata kama kila mtu anaukubali kama ukweli. Na ukweli huwa unabaki kuwa ukweli hata kama kila mtu anaukataa. Hivyo kamwe usiangalie watu kwenye maisha yako, bali angalia misingi na sheria za asili. Kama kitu kinaenda kinyume na hayo, jua siyo sahihi, haijalishi wangapi wanakubaliana nacho.
Watu wengi hujiingiza kwenye matatizo makubwa kwa sababu ya tamaa na wivu, tamaa ya kupata vitu kwa haraka na wivu wa kuona wengine wananufaika kuliko wao.
Matapeli wote wanajua wengi huanguka kwenye vitu hivyo viwili, hivyo mipango yao ya utapeli hujaza tamaa na wivu, wanakuonesha jinsi ilivyo rahisi kufanikiwa na wanakupa uhakika kabisa, huku wakikuonesha wengine ambao wamefanikiwa kwa njia hiyo.
Unahitaji msingi imara kuweza kuvuka viunzi, msingi ambao wengi hawana na ndiyo maana wanaanguka. Kwa kuwa ndani ya KISIMA CHA MAARIFA na kuyapata mafunzo haya ya kila siku, unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuvuka hali hizo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,