Watu wengi wamekuwa wanajiambia wanaanzisha biashara mpya kwa sababu wameona fursa fulani mahali.

Lakini ukweli siyo wanaanzisha biashara mpya, bali wanakwenda kuiga biashara nyingine inayofanyika eneo hilo au kuhamisha biashara kutoka eneo jingine kwenda hapo.

Hivyo biashara wanayokwenda kuanzisha siyo ya tofauti wala ya kipekee sana. Na hapo wanakuwa wamejipeleka wenyewe kwenye ushindani au kukaribisha ushindani.

Kama umeona mahali kumekosa huduma fulani ambayo watu wanaihitaji na ukaenda kuianzisha kwa namna huduma hiyo inapatikana maeneo mengine, hapo umehamisha biashara kutoka eneo moja kwenda jingine. Hakuna kinachoweza kumzuia mtu mwingine kufanya kama wewe.

Kama umeona eneo kuna biashara fulani, lakini kuna vitu wateja hawapati na wewe kuchagua kwenda kuanzisha biashara eneo hilo, inayotoa kile wateja wanakosa sasa, unaenda kuleta maboresho kwa asilimia fulani, huna cha kukutofautisha na mwingine atakayeanzisha biashara kama yako.

Kwa njia hizi, wengi wamekuwa wanaingia kwenye biashara ambayo tayari ina ushindani au inayokaribisha ushindani kwa urahisi. Kwa sababu biashara wanayoanzisha ni rahisi, inayoweza kuanzishwa na kila mtu.

Peter Thiel kwenye kitabu chake cha Zero To One, ambapo ameshirikisha siri nyingi za kuanzisha biashara mpya, anaeleza hakuna kitu cha hovyo kama kuingia kwenye biashara yenye ushindani.

Japokuwa wengi wanaamini mfumo wa uchumi wa ubepari unataka ushindani, Thiel anasema kama unataka kufanikiwa kwenye biashara, kitu cha kwanza kuondokana nacho kabisa ni ushindani.

Sasa unajitofautishaje na ushindani kwenye aina ya uchumi ambao kila mtu yuko huru kuanzisha biashara ya aina yoyote ile?

Thiel anatuambia ni kwa kuanzisha biashara ya tofauti kabisa, siyo inayofanana na zilizopo sasa, wala yenye maboresho kwa asilimia 10, bali biashara ambayo ina maboresho mara 10 ya biashara zilizopo sasa.

Yaani biashara ambayo ni ya tofauti kabisa, ambayo hakuna mtu amewahi kufikiria kuianzisha, na ukishaianzisha basi unaliteka soko mapema kiasi kwamba washindani wakitaka kuingia, wanakosa pa kuanzia.

Ni rahisi kusema kwamba hakuna wazo jipya la biashara, kila wazo limeshafanyiwa kazi na huwezi kuja na kitu kipya kabisa.

Lakini ukiangalia jinsi fursa mpya za kibiashara zinaanzishwa kila siku, hasa kwa ukuaji wa teknolojia, unaona jinsi mambo ambayo yalikuwa yanaonekana ni ya kawaida yameweza kuwa mawazo bora ya kibiashara.

Nani alifikiri siku moja kuuza vitabu mtandaoni (amazon) itakuwa biashara kubwa, au unaweza kuwapa watu lifti kwenye gari lako na wakakulipa (uber), au kama una chumba cha ziada na usichotumia nyumbani kwako unaweza kupangishia watu kwa muda kama hoteli (air bnb), au kufuatilia maisha ya watu mtandaoni (facebook/instagram) kunaweza kuingiza kipato kikubwa?

Hayo ni baadhi ya mawazo ambayo hakuna aliyejua yangeweza kulipa, mpaka yalipoanza kufanyika na watu kunufaika. Unaweza kuwa na wazo sasa na ukajiambia ni la kijinga, lakini ukiamua kulifanyia kazi na kuangalia jinsi unavyoweza kutoa thamani kwa wengine, una nafasi ya kuja na kitu cha tofauti na kitakachokuondoa kabisa kwenye ushindani.

Kumbuka usiwe bora kwa asilimia 10, kuwa bora mara 10 kabisa, kwa kuja na kitu kipya, kitu ambacho wengine hawajawahi kukifikiria, lakini kinaweza kuongeza thamani kubwa kwenye maisha yao.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha