There are two ways not to suffer from poverty. The first is to acquire more wealth. The second is to limit your requirements. The first is not always in our power but the second is always in our power.” — Indian proverb
Kuna njia kuu mbili za kutokusumbuliwa na umasikini.
Njia ya kwanza ni kutengeneza utajiri mkubwa sana, ambao hautatikiswa na umasikini wowote.
Njia ya pili ni kudhibiti mahitaji na matumizi yako.
Njia ya kwanza ni nzuri, lakini siyo mara zote inakuwa ndani ya uwezo wako.
Unaweza kutengeneza utajiri mkubwa, lakini mambo ya nje yakapelekea utajiri huo kuanguka.
Njia ya pili iko ndani ya uwezo wako kabisa, unapodhibiti tamaa na matakwa yako, unapoendelea kubaki na mahitaji ya msingi tu hata ukiwa na utajiri mkubwa, umasikini haukusumbui.
Kwa walio wengi, kadiri wanavyopata utajiri, ndivyo hatari ya umasikini inawasumbua.
Hii ni kwa sababu wengi huruhusu mahitaji na matumizi yao kukua kadiri utajiri wao unavyokua.
Hivyo wanajikuta kwenye mtego mkali, wana utajiri mkubwa, lakini kwa mahitaji na matumizi waliyonayo, chochote kikitokea kwenye utajiri wao, maisha yao yatakuwa ya mateso sana.
Wengi hufikiri utajiri unawapa uhuru pale wanapoweza kupata kila walichotaka na ndiyo maana wanaruhusu mahitaji yao kuendelea kukua kadiri utajiri unavyokua.
Hawataki kudhibiti mahitaji yao kwa sababu wanaona kufanya hivyo ni kujinyima uhuru, wanajiambia ya nini kuwa na fedha na utajiri kama huwezi kuvitumia utakavyo?
Kutumia utakavyo fedha na utajiri wako siyo uhuru, bali ni kujiweka kwenye utumwa, maana utafika mahali na kuwa mtu wa kuhofia maisha yatakuwaje iwapo utajiri wako utapotea.
Lakini ukiwa na fedha na utajiri, huku ukiendelea kujidhibiti wewe mwenyewe kwenye matakwa, tamaa na matumizi, unazidi kuwa huru. Hutakuwa na hofu yoyote kuhusu utajiri kupotea, kwa sababu unajua maisha yako hayatakwama.
Kwa nje watu watakuona bahili na kukusema vibaya, lakini ndani yako una uhuru mkubwa wa kuishi maisha bora kwako badala ya kuwa na hofu kila siku.
Hivyo anza kwa kudhibiti tamaa, matakwa na matumizi yako, kisha pambana kuongeza kipato chako kadiri uwezavyo.
Na hata kipato kiongezeke kiasi gani, usipoteze udhibiti wako binafsi.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu siyo asilimia 10, bali mara kumi, sona zaidi hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/10/01/2101
Rafiki yako,
Kocha Dr Makirita Amani.