Kila mtu huwa anasambaza kile kilicho ndani yake, hakuna anayependa kukaa na kitu ndani yake.
Hivyo wale wenye hofu, huwa wanasambaza hofu hiyo kwa wengi zaidi.
Na wenye maumivu huwa wanahakikisha wanawapa watu wengi maumivu hayo.
Kadhalika wanaoteseka, huwa wanahakikisha kuwatesa wengine.
Na wale wenye upendo, huwa wanawapenda zaidi wengine.
Kwa kujua hili, kuna mambo matatu unanufaika nayo;
Moja ni kujawa na yaliyo mazuri ili uweze kuyasambaza kwa wengine. Huwezi kutoa kitu ambacho huna. Hivyo kama unataka kuwapenda wengine, anza kuwa na upendo ndani yako.
Mbili ni kuwaelewa watu, kwamba yale wanayofanya siyo makusudi, bali ndiyo walivyo. Hii itakufanya uwaonee huruma badala ya kuwalaumu. Kama kuna mtu anakutesa, badala ya kulalamika anakutesa unamuonea huruma kwa mateso ambayo amekuwa anaishi nayo miaka yote.
Tatu ni kuwa makini na watu ambao unajihusisha nao. Ili kuzijua tabia halisi za mtu, angalia jinsi anavyojihusisha na wengine, hasa wale ambao ana mamlaka juu yao, wale ambao anaweza kufanya chochote kwao. Hiyo itakupa picha halisi ya mtu na utajua kama ni mtu unayetaka kujihusisha naye au la.
Watu huwa wanatoa kile kilicho ndani yao, hivyo usishangae kwa nini mtu anafanya kitu fulani, bali jua hivyo ndivyo alivyo ndani yake.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante sana Kocha kwa makala nzuri.
LikeLike