“Nguvu kubwa inayouendesha ulimwengu ipo ndani yangu. Chochote ninachotaka kwa imani hai, mategemeo chanya na nia thabiti kiko njiani kuja kwangu. Na kama kile ninachotaka hakijaja, basi ni kwa sababu kuna kikubwa na bora zaidi kipo njiani kuja kwangu. Ninajua imani hii ni ya kweli na nitaisimamia mara zote.”

Kauli hii, ina nguvu kubwa pale unapojiambia kila mara na kuiishi, hujiambii tu kujifurahisha, bali unajiambia kwa kuiamini na kuiishi, kwa kuchukua hatua sahihi zinazoendana na kauli hiyo, na hapo ndipo ulimwengu utakupa kile unachotaka.

Tukiichambua zaidi kauli hii, kuna ya msingi sana kuelewa na kuyazingatia, ili isiwe tu unajiambia kujifurahisha.

Kwanza kabisa lazima ujue ndani yako kuna nguvu kubwa, kubwa kuliko ambavyo umekuwa unaitumia sasa, hilo lazima uliamini na kulifanyia kazi.

Pili ni lazima ujue nini hasa unachotaka, na uwe tayari kujitoa kweli kukipata. Usiwe unabahatisha au kutamani, amua nini unataka na kuwa tayari kufanya chochote ili kukipata.

Tatu ni kuwa na imani hai, imani inayotoka ndani yako na siyo ya kuiga, kujishawishi bila ya shaka yoyote kwamba utapata kile unachotaka.

Nne ni kuwa na fikra na mategemeo chanya, kuondokana kabisa na hali zozote hasi.

Tano ni kujua hujakosa, hata kama hujapata kile ulichokuwa unataka, hujakosa, bali kuna kikubwa na bora zaidi kipo njiani kinakuja kwako. Muhimu ni wewe usipoteze imani wala kuwa na mtazamo hasi.

Imani ina nguvu kubwa ya kutusukuma, hasa pale inapoanzia ndani yetu na ikiwa na ushahidi wetu binafsi. Jijengee imani hii na utaweza kufanya makubwa kwenye maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha