Watu wengi hufanya kilicho sahihi kwa sababu wana ajenda fulani, kuna kitu wanategemea kukipata kwa kufanya kilicho sahihi.

Hivyo wengi hufanya kilicho sahihi kama maigizo, haitoki kweli ndani yao, bali wanafanya kwa mategemeo fulani.

Lakini Mstoa Marcus Aurelius alituasa vyema, sababu pekee ya kufanya kilicho sahihi ni kwa kuwa ndiyo kitu sahihi kufanya.

Sijui umeelewa vizuri hapo rafiki yangu au unahitaji muda ili izame vyema, unafanya kilicho sahihi, siyo ili uonekane, au ulipwe kwa wema uliofanya, bali kwa sababu ndiyo kitu sahihi kufanya.

Mahali pengine Marcus alituonya kuhusu kusubiri shukrani pale tunapotenda kwa wengine. Alitueleza wazi kwamba faida ya kutenda wema tumeshaipata kwa kutenda wema huo, kusubiri shukrani ni kuharibu ole faida ambayo unakuwa umeshaipata.

Fanya kilicho sahihi kwa sababu ndiyo kitu sahihi kwako kufanya, huwezi kufanya mbadala na hicho sahihi. Fanya wema kwa sababu ndiyo namna sahihi kwako kuishi, huwezi kuishi kinyume na hivyo.

Kwa kifupi, kwa chochote unachofanya, kifanye kwa sababu ndiyo msingi wako wa maisha, na siyo kwa sababu unataka kuonekana au kuna kitu unategemea kupata kwa kufanya kitu hicho.

Kwa kuishi maisha yako hivi, utaondokana na msongo mwingi unaoletwa na mategemeo hewa ambayo wengi wamekuwa wanajijengea.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha