Mtu mmoja amewahi kusema kama watu wanaoishi sasa watachukuliwa na kurudishwa kwenye aina ya maisha ambayo watu waliishi kwenye karne ya kwanza, basi karibu wote watafariki kwa haraka sana.

Hii ni kwa sababu mazingira ya sasa ni rahisi sana ukilinganisha na mazingira ya kipindi hicho. Mazingira hayo rahisi yamefanya sehemu kubwa ya watu kuwa laini laini, kiasi kwamba mambo yakibadilika, hawataweza kuhimili.

Sasa siyo tu kubadilika kwa mambo ndiyo kunaathiri kizazi hiki, bali hata kufikia mafanikio kunaathiriwa sana. Kutokana na ulaini wa watu wa sasa, hawajisukumi tena kufanya makubwa.

Watu wanashauriwa kujali mambo madogo madogo na ya hovyo, yasiyo na mchango wowote kwao. Watoto wanalelewa kimayai, kwa kuahidiwa kwamba watapata makubwa hata kama hawafanyi makubwa.

Jamii inazuia watu wasiumie iwe ni kimwili, kiakili au kiroho. Watoto wanalelewa kwenye mazingira ya kuchungwa sana. Na hata watu wazima wana njia nyingi za kuwalinda. Lakini ulinzi wote huo umezalisha watu wasioweza kupambana na makubwa.

Jamii inapenda watu wa aina hiyo, ukishakuwa laini, jamii inakutumia utakavyo, maana huwezi kusimama mwenyewe. Unapokuwa chini ya jamii, hakuna namna unaweza kufanikiwa, maana utafanya kile ambacho kila mtu anafanya.

Tumezalisha kizazi cha watu laini, watu ambao hawawezi kujisukuma zaidi ya ukomo wao, watu ambao hawawezi kutimiza kile wanachoahidi, hata mipango yao wenyewe, wanapokutana na ugumu wanakata tamaa na kukimbia.

Kama unataka kuwa na maisha yako, kama unataka kufanya makubwa na kufanikiwa, lazima kwanza ukatae kuhadaiwa na jamii, lazima ukatae usalama uliopitiliza ambao jamii inakuhadaa nao na lazima uwe tayari kujiweka kwenye hali za hatari ili kufanya makubwa.

Kama unachotaka kwenye maisha yako ni usalama wa asilimia 100, nenda kakae jela, maana huko unalindwa na kulishwa hata kama hufanyi chochote ila hutakuwa huru. Jamii haina tofauti na jela, maana ukishaambatana nayo, unapoteza uhuru wako. Kama unataka kuwa huru na maisha yako, lazima uwe tayari kusimama mwenyewe, lazima uwe tayari kukabiliana na hatari. Mambo hayatakuwa rahisi, lakini matokeo utakayoyapata yatakuwa bora sana.

Usihadaie na ulaini ambao jamii inakuandalia, tambua huo ni kwa wanaotaka kuwa kawaida, wewe unayetaka kuwa zaidi ya kawaida, lazima upambane hasa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha