Watu wamekuwa wanatumia nguvu nyingi kwenye mbwembwe kuliko kwenye kazi.

Kwenye maonesho kwamba wanafanya kazi kuliko kazi yenyewe wanayoifanya.

Wengi wanakazana ili waonekane wanafanya kazi, ili waonekane wako ‘bize’ lakini hakuna chochote kikubwa wanachozalisha.

Na haya yote yamechochewa na ukuaji wa mitandao ya kijamii, maana hiyo inampa kila mtu nafasi ya kuitangazia dunia nzima kuhusu yeye.

Kama kweli watu wangekuwa wanafanya kazi kama wanavyofanya maonesho ya kazi, wangeweza kupiga hatua kubwa sana.

Lakini wengi hawafanyi kazi, wapo kwenye maonesho zaidi.

Wewe ondoka kwenye hilo, achana na mbwembwe na weka kazi. Fanya kazi yako kwa ubora wa hali ya juu, kwa kuweka kila unachoweza kuweka ili kazi hiyo iwe bora na matokeo yataweka mbwembwe yenyewe.

Utashawishiwa kwamba usipoonesha kazi yako watu hawatakujua, utaambiwa bila mbwembwe hupati matokeo mazuri, lakini hayo yote ni uongo.

Kitu pekee cha uhakika kinachoweza kukuwezesha kufahamika kwa kazi yako na kuwafikia wale muhimu ni kazi yenyewe. Weka kazi, kwa ubora wa hali ya juu sana na utaweza kupiga hatua kubwa.

Kipaumbele cha kwanza kazi, acha matokeo ya kazi yako ndiyo yalete mbwembwe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha