Wakati nasoma shule ya sekondari, kwenye somo la Kiingereza kulikuwa na vitabu vya fasihi na ushairi ambavyo vilikuwa kwenye mtaala, ambavyo kila mwanafunzi alipaswa kuvisoma na kwenye mitihani kulikuwa na maswali ya kujibu kutokana na vitabu hivyo.
Mwalimu wetu wa Kiingereza alitufundisha vitabu viwili tu na kuamini hivyo vingekuwa msaada kwetu kujibu maswali ya mtihani. Lakini kulikuwa na vitabu zaidi ya sita kwenye mtaala, na vyote vilikuwepo shuleni. Sasa kwa kuwa nilikuwa napenda kusoma vitabu tangu zamani, nilikuwa namuomba mwalimu vitabu hivyo na kuvisoma.
Hivyo nilikuwa nimesoma vitabu vingi vya fasihi ya Kiingereza na siku ya mtihani wa mwisho, nilikuwa na uwanja mpana wa kuchagua nitumie kitabu kipi kwenye kujibu maswali. Hilo liliniwezesha kupata ufaulu wa juu kwenye somo hilo kwa alama A.
Sasa kikubwa kilichonisaidia siyo tu kujua vitabu vingi, bali kuvisoma. Kwani hata wanafunzi wengine walijua vitabu vingine vya ziada, ila wao walikuwa wamesoma muhtasari wa vitabu hivyo, ambapo kulikuwa na wengi wameandaa muhtasari na ufupisho wa kila kitabu.
Wakati wao wanakariri ufupisho wa vitabu, mimi nilikuwa nimevisoma vitabu vyenyewe, kwa hiyo nilikuwa na uwanja mpana wa kuelewa na kuweza kutumia kwenye kujibu mtihani. Lakini hilo pia liliimarisha tabia yangu ya kupenda kujisomea ambayo imekuwa na msaada mkubwa kwenye maisha yako.
Sasa ujumbe mkuu kwako leo rafiki yangu ni kuhusu utamaduni mpya uliojengeka kwa wengi sasa, utamaduni wa kupenda vitu vya kutafuniwa. Watu wengi sasa hawataki kusoma vitabu bali muhtasari au uchambuzi wa vitabu hivyo. Watu wengi hawana hata muda wa kusoma makala ndefu, wanataka maneno mafupi ya kwenye mitandao ya kijamii.
Ingia kwenye mtandao wowote wa kijamii, angalia jumbe ambazo watu wanaweka kwenye mtandao wa wasap (status) utaona watu wanaweka jumbe nzuri mno, jumbe za hekima kubwa. Lakini mbona hawaendeshi maisha yao kwa namna hiyo?
Jibu unakuja kujua ni kwamba wamekariri tu, wamebeba tu, wametafuniwa na wao wanameza. Hivyo hawaelewi, hawabadiliki kwa sababu hawajaingia kwa kina kwenye kitu husika.
Wito wangu kwako ni huu, mara zote penda kurudi kwenye chanzo kikuu, rudi kwenye kusoma vitabu. Soma jumbe fupi uwezavyo, soma muhtasari na chambuzi utakavyo, lakini usiondoe nafasi ya wewe kusoma vitabu husika.
Nimekuwa nachambua vitabu kwa muda mrefu sasa, najua wengi wananufaika na hilo, lakini hawapaswi kutokusoma vitabu husika. Unaweza usiweze kusoma vyote, lakini hakikisha kuna vichache unachagua kusoma.
Uchambuzi wa vitabu ambao nimekuwa nafanya, siyo tu kwa ajili ya wengine, bali pia ni kwa ajili yangu, ninapochambua kitabu, ninakielewa zaidi kuliko nisipokichambua. Wakati mwingine nalazimika kurudi kwenye kitabu kama kuna kitu sijaelewa. Na pia inakuwa njia rahisi kwangu kurejea kitabu ambacho nilishasoma. Nikiwa nimesoma kitabu na nikaja kusoma uchambuzi wake, naelewa vizuri kuliko kusoma uchambuzi pekee.
Hivyo usipende vitu vya kutafuniwa, penda kutafuna mwenyewe.
Kila mtu sasa anatafuta vitu rahisi, tambua kwenye urahisi thamani siyo kubwa. Wewe nenda kwenye ugumu, tafuna mwenyewe na juhudi unazoweka zitakufanya uelewe zaidi na pia ubadilike.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Uvivu ndio chanzo cha mtu kupenda kumeza tu pasipo kutafuna mwenyewe.
Asante Kocha.
LikeLike
Karibu Datius
LikeLike