Simu ya Iphone iko kwenye toleo la 12, wakati toleo la kwanza linatoka, ilikuwa ni mapinduzi makubwa mno kwenye ulimwengu wa teknolojia na mawasiliano. Ilikuwa ni kitu ambacho hakijawahi kuonekana wala kudhaniwa na ilibadili kabisa maisha ya watu.
Ingetosha kwa kampuni ya Apple kusema wamemaliza, wameweza kuleta mapinduzi makubwa na hawahitaji kufanya kitu kingine zaidi, bali kusambaza simu hiyo kwa wengi.
Lakini haikuwa hivyo, karibu kila mwaka kuna toleo jipya la simu hiyo linatoka, ambalo ni bora kuliko lililopita. Ukilinganisha toleo la 12 na la kwanza au hata la 4 ni vitu tofauti kabisa, matoleo hayo yanatofautiana mno.
Kampuni ya Apple inajua siri moja ambayo iliachiwa na aliyekuwa muasisi wake, Steve Jobs, ambaye alisema ukitengeneza kitu kizuri, usikae na kuona umeshamaliza kazi, bali nenda katengeneze kitu kingine kizuri zaidi ya hicho. Hiyo ndiyo njia pekee ya kubaki kwenye soko na mafanikio ya juu.
Hilo linafanya kazi kwenye kila sekta,
Hakuna mwandishi mwenye mafanikio ambaye ameandika kitabu kimoja pekee, waandishi wote wenye mafanikio wameandika vitabu vingi.
Hakuna mwanamuziki mwenye mafanikio ambaye ametoa wimbo mmoja pekee, bali wametoa nyimbo nyingi.
Hakuna mjasiriamali mwenye mafanikio ambaye ameanzisha biashara moja na kuiendesha kwa mazoea. Bali wajasiriamali wote wenye mafanikio wameanzisha biashara zaidi ya moja na kuzikuza kadiri muda unavyokwenda.
Unapopanga mafanikio yako, jua kabisa hakuna chochote utakachofanya mara moja na kikakupa mafanikio ya kudumu. Lazima kila wakati uwe tayari kufanya kwa ubora zaidi.
Ukifanya kitu kizuri na watu wakakipokea vyema, usibweteke na kuona umeshamaliza, anza kutengeneza kingine ambacho ni bora zaidi ya hicho. Kwa sababu usipofanya hivyo wewe mwenyewe, kuna wengine wanafanya hivyo. Ukijiambia umeshamaliza, kuna wenzio ndiyo kwanza wanaanza na lengo lao ni kuchukua nafasi uliyonayo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asilimia kubwa ya walio wengi wakisha piga hatua kidogo wanaridhikia na hawajisumbiui tena kufanya zaidi. Kumbe hawajui kuwa wanajitengenezea anguko kubwa.
Asante sana kocha kwa makala nzuri.
LikeLike
Ni kweli Datius, wengi wanajikwamisha na kujiangusha wenyewe.
LikeLike