Watu waliopo kwenye safari ya kuelekea kwenye utajiri ni wengi, lakini kati yao, wachache ndiyo wanaofika kwenye utajiri.
Na katika kundi la wale wanaofika kwenye utajiri, ni wachache ambao hudumu na utajiri huo. Wengi huupata utajiri na baadaye kuwapotea, kuanguka kutoka kwenye utajiri.
Wale wanaoshindwa kufika kwenye utajiri ni kwa sababu hawana misingi sahihi ya kuwafikisha kwenye utajiri. Wengi huhangaika na njia za mkato ambazo ni za kubahatisha na hazizalishi utajiri.
Hivyo kwenye safari ya kufika kwenye utajiri, kwanza hakikisha kuna thamani kubwa unayozalisha kwa ajili ya wengine, ambayo wako tayari kulipia ili kuipata.
Thamani hiyo asiwepo mwingine duniani anayeweza kuizalisha kama wewe, ni wewe tu na hivyo hakuna anayeweza kushindana na wewe na dunia haina budi kukulipa kwa thamani hiyo isiyopatikana kwa mwingine yeyote.
Hapo tu unaweza kuona kwa nini wengi hawafiki kwenye utajiri, kwa sababu kile wanachofanya kinaweza kufanywa na wengine wengi, hivyo wanakuwa na ushindani mkali na hawawezi kuipangia dunia iwalipe nini, dunia ndiyo itapanga ilipe kiasi gani.
Msingi huu ni muhimu mno, hakikisha kuna thamani unayozalisha, ambayo hakuna mtu mwingine duniani anayeweza kuizalisha, na dunia inaihitaji sana kiasi cha kuwa tayari kuilipia, wewe ndiye unayepanga bei na hakuna mshindani.
Kwa kufuata msingi huo, lazima utafika kwenye utajiri, lakini kubaki kwenye utajiri, unahitaji msingi mwingine muhimu, ambao wengi huwa wanaukosa.
Msingi ambao utakufanya uendelee kudumu kwenye utajiri unaotengeneza ni huu; kwenye kila kipato chako weka akiba, kisha iwekeze akiba hiyo mahali ambapo inazalisha kipato cha ziada na thamani yake inakua kadiri muda unavyokwenda.
Kwa kifupi msingi wa pili ni kuhakikisha unawekeza, lakini siyo kuwekeza tu kiholela, bali kuwekeza sehemu ambapo kuna faida inazalishwa na kadiri muda unavyokwenda thamani ya uwekezaji wako inakua.
Nadhani unaona mwenyewe ni jinsi gani utafika na kubaki kwenye utajiri, kwa sababu unafanya kitu cha tofauti ambacho huna mpinzani, unalipwa vizuri, sehemu kubwa ya kipato unachopata unakiwekeza eneo ambalo linazalisha faida na thamani kukua.
Hakuna namna utafuata misingi hii miwili kwa uaminifu na subira na ukashindwa kufikia lengo.
Kama unajiuliza ni thamani gani ya tofauti unayoweza kuzalisha, kama unatafuta wa kukufundisha hilo, tayari umeshashindwa, hiyo inapaswa kutoka ndani yako mwenyewe. Kama kuna anayeweza kukufundisha, basi jua ataweza kuwafundisha wengine na hapo utakosa ule upekee.
Fanyia kazi misingi hii miwili, kaa kwenye njia sahihi na jipe muda, kwa hakika utafika na kudumu kwenye utajiri.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,