Watu huwa wanalalamikia hamasa wanazopata kutoka kwa wengine zimekuwa hazidumu.

Mfano mtu anahudhuria semina au kusoma kitabu na kuhamasika sana, anatoka akiwa na mipango mikubwa ya kwenda kubadili kabisa maisha yake.

Lakini siku chache baadaye hamasa ile inakuwa imeisha kabisa na kurudi kwenye mazoea.

Wengi hufikiri tatizo liko kwenye hamasa wanazopata, lakini ukweli ni tatizo lipo ndani yao wenyewe.

Watu wanapohamasika, huwa wanaweka mipango mikubwa, ambayo kwa hamasa waliyonayo mwanzo wanasukumwa kuifanyia kazi. Lakini siku zinavyokwenda wanachoka, mambo waliyopanga ni makubwa mno.

Uchovu wanaoupata unawapelekea kuachana na makubwa waliyopanga na kurudi kwenye mazoea.

Kuondokana na hali hii ya kuanza na kuacha, weka mipango ambayo unaweza kwenda nayo muda mrefu. Hata kama umehamasika kiasi gani, usiweke mipango ambayo itakuchosha haraka, badala yake weka mipango ambayo utaweza kuchukua hatua kila siku kwa muda mrefu.

Unaweza kuweka mpango mkubwa unaokusukuma kukesha kwa siku chache na ukapiga hatua, lakini baada ya hapo utakuwa umechoka sana kiasi kwamba huwezi kuendelea tena.

Lakini unaweza kuweka mpango huo huo mkubwa na kuweka hatua ndogo za kuchukua kila siku na ukachukua hatua hizo kwa miaka mingi, ukapata matokeo makubwa na usichoke.

Haijalishi umehamasika kiasi gani, mambo yote mazuri yanahitaji muda, mtu anayebeba ujauzito, hata kama ana hamasa kiasi gani, ujauzito haukamiliki mpaka miezi tisa. Hivyo na wewe kwenye mpango wowote unaojiwekea, jipe muda wa kutosha na hakikisha unaweza kuendelea na safari hiyo kwa muda mrefu.

Muda mfupi kabisa wa kujiwekea ni miaka 10, hivyo kwa kila unachopanga, jiulize unaweza kuendelea kukifanya kwa miaka kumi? Kama huwezi bora upange upya, kwa sababu kuendelea na mpango ambao huwezi kwenda nao miaka kumi, ni kujiandaa kuchoka na kuishia njiani.

Mafanikio yamekuwa magumu kwa wengi siyo kwa sababu hawana mipango mikubwa na kuchukua hatua, bali wanayo mipango na hatua wanachukua, ila hatua zao hazidumu, wanachoka haraka na kupotea.

Wewe epuka hili kwa kuhakikisha unaweka mipango na hatua za kuchukua ambazo unaweza kwenda nazo kwa angalau miaka kumi bila ya kuchoka. Na hapo lazima kiwe kitu unachokipenda na kukipangilia kwa namna unapata muda wa kupumzika vizuri.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha