Watu wote ambao walileta mapinduzi na mabadiliko makubwa kwenye kila eneo la maisha, ambayo tunayafurahia sasa, hawakukubalika kirahisi. Walipingwa, wakateswa na wengine kuuawa kwa sababu tu walifikiri tofauti na kundi kubwa lilivyokuwa linafikiri.
Kwa upande wa falsafa, Socrates alikuja na njia mpya ya kuwajengea watu uwezo wa kufikiri, kuhoji na kujifunza badala ya kukubali tu kile wanachoambiwa au walichozoea, kilichotokea ni alipingwa na kuhukumiwa kifo. Leo tunamkumbuka Socrates na kujifunza kwake, lakini hatuwajui wale waliompinga na kumhukumu.
Kwenye sayansi Galileo alifikiri na kuhoji tofauti, akapata ushahidi kwamba siyo jua linazunguka dunia, bali dunia inazunguka jua. Hii ilikuwa kinyume kabisa na ilivyozoeleka, hivyo alipokuja na hayo ya tofauti alipingwa, kufungwa na hata kuuawa. Leo hii tunamjua na kujifunza kupitia Galileo, wakati waliompinga wengi hatuwajui kabisa.
Mifano ni mingi, wagunduzi wa teknolojia mbalimbali, mwanzoni walipitia magumu, walikataliwa, walipingwa, walifungwa na wengine kuuawa, lakini leo tunawajua wagunduzi hao, huku wapingaji tukiwa hatuwajui kabisa, dunia imewasahau.
Ninachotaka kukuambia wewe rafiki yangu ni kwamba safari ya mafanikio siyo rahisi, kwa sababu mafanikio yanakutaka uwe tofauti, ufanye ambacho hakijazoeleka na wengine na hapo lazima utapingwa vibaya.
Lakini lipo tumaini kubwa, kwamba mwisho wa siku, dunia itawasahau wale wote wanaokupinga na itakukumbuka wewe kama utasimamia kile cha tofauti unachofanya na chenye manufaa kwa wengine.
Haijawahi kuwa rahisi na haitakuwa rahisi kwako, hivyo jiandae na ujitoe, ukijua mbele yako kuna kazi mara mbili, ya kwanza kufanya kile unachofanya na ya pili kukabiliana na jamii ambayo haitaki kabisa kukuruhusu ufanye unachotaka.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Shukrani sana Kocha,kwa makala hii.
LikeLike
Karibu Datius
LikeLike