“The most important knowledge is that which guides the way you lead your life.” – Leo Tolstoy
Tunaishi kwenye zama za mafuriko ya maarifa na taarifa.
Vitabu vilivyoandikwa ni vingi mno, kiasi kwamba hakuna anayeweza kusoma hata asilimia 1 tu ya vitabu vyote.
Makala, video na sauti zenye mafunzo mbalimbali ni nyingi.
Walimu na washauri nao pia ni wengi.
Tunatamani mno kupata maarifa kwa wingi tuwezavyo, lakini muda na nguvu ni kikwazo kikubwa kwetu.
Je tunachaguaje maarifa yaliyo muhimu kwetu na kuhangaika nayo huku tukipuuza yasiyo muhimu?
Jibu ni kuangalia ni jinsi gani unaweza kuyatumia maarifa hayo kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.
Maarifa yaliyo sahihi kwako ni yale yanayokupa mwongozo sahihi wa hatua za kuchukua ili kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Hivyo cha kwanza kabisa ni lazima ujue nini unachotaka, wapi unapotaka kufika.
Halafu sasa unayatafuta maarifa yatakayokuongoza vizuri, unawachagua walimu na washauri watakaokusaidia kufika unakotaka.
Na kadiri unavyokwenda na safari yako, utakutana na changamoto mbalimbali, hizo pia zinakuonesha ni maeneo gani hujawa imara na hivyo kuhitaji maarifa zaidi.
Usikubali kuzama kwenye mafuriko ya maarifa na taarifa tuliyopo sasa.
Chagua maarifa na taarifa sahihi kwako kwa kuzingatia kule unakotaka kufika.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu chanzo kikuu cha msongo, soma hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/11/16/2147
Rafiki yako,
Kocha Dr Makirita Amani.