Upo usemi maarufu kwenye biashara kwamba unaweza kuwa rahisi au haraka au bora, lakini unaweza kufanya viwili tu kwa wakati mmoja na siyo vyote vitatu. Hivyo unapaswa kuchagua viwili ambavyo utapambana navyo kwenye biashara yako.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye mafanikio kwenye kila eneo la maisha, kupitia chochote unachokifanya.

Unaweza kuwa ndiye unayefanya kwa bei rahisi kuliko wengine wote, na hapo utawavutia wengi kuja kwako kwa sababu bei yako ni rahisi.

Au unaweza kuwa ndiye unayefanya kwa haraka kuliko wengine wote, watu wanajua wakija kwako hawapotezi muda mwingi.

Au unaweza kuwa ndiye unayefanya kwa ubora kuliko wengine wote, watu wanajua wakija kwako kazi ni bora kabisa.

Ukiwa rahisi, utawavutia wengi, hivyo hata kama unafanya kwa haraka, wingi wa watu utazuia haraka hiyo isiwezekane na kama ikiwezekana basi ubora lazima upungue.

Hivyo kama unachojali cha kwanza ni urahisi, basi lazima uwe tayari kuachana na kimoja, haraka au ubora. Itabidi uchague kufanya kwa haraka lakini usijali ubora au ujali ubora lakini usifanye haraka.

Kama umechagua haraka kuwa kigezo chako kikuu, lazima uchague kimoja utakachoachana nacho, kama utataka ufanye kwa ubora basi jua bei lazima iwe juu na kama utataka uendelee kuwa rahisi basi jua ubora utakuwa chini.

Kadhalika kama umechagua ubora kuwa kigezo chako kikuu, inabidi uchague kufanya kwa bei ghali kama unataka ufanye kwa haraka au kwa bei rahisi lakini uwe tayari kuchelewa.

Unaweza kuchagua viwili tu kati ya hivyo vitatu, hivyo jua ni vipi unavyochagua wewe na tengeneza kile unachofanya katika msingi huo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha