Peter Thiel kwenye kitabu chake cha ZERO TO ONE aliandika; “Kila wakati kwenye biashara huwa unatokea mara moja tu. Bill Gates ajaye hataanzisha mfumo wa kompyuta, Larry Page na Sergey Brin wajao hawataanzisha mfumo wa kutafuta vitu mtandaoni. Na Mark Zuckerberg ajaye hataanzisha mtandao wa kijamii. Kama unawaiga watu hao, hujifunzi kutoka kwao.”

Hii ni kauli nzito na iliyobeba ujumbe mkubwa sana ambao mtu akiuelewa na kuufanyia kazi, ataondoka kwenye uongo mwingi ambao jamii imekuwa inalishwa na kuwazuia watu kufanikiwa.

Kuna mamilioni ya vitabu yaliyoandikwa kuhusu watu waliofikia mafanikio makubwa sana kwenye maisha yao, lakini vitabu hivyo havijaweza kuzalisha watu wapya wenye mafanikio makubwa.

Hiyo ni kwa sababu hadithi za mafanikio zinazoshirikishwa kupitia vitabu na njia nyingine, zimekuwa kikwazo kwa wale wanaojifunza kuweza nao kufanikiwa.

Tatizo kubwa ambalo linafanya hadithi za mafanikio zisiwe na msaada kwa wale wanaozipata ni kufikiri wakifanya kila ambacho wale waliofanikiwa walifanya, basi nao watafanikiwa.

Hivyo unakuta watu kila siku wanajaribu vitu vipya.

Mtu anasoma walioanikiwa wanaamka mapema, anaanza kuamka mapema. Anasoma tena waliofanikiwa wanachelewa kulala, anaanza kuchelewa kulala. Mafunzo hayo mawili tu yanakinzana, huwezi kuchelewa kulala na ukawahi kuamka, mtu anapojaribu kufanya vyote, anaishia kushindwa kabisa. Ambacho mtu angepaswa kuelewa hapa ni kwamba wale waliofanikiwa sana, huwa wanakuwa na muda mwingi kwa ajili ya kufanya mambo yao, muda ambao hawasumbuliwi na wengine. Na huwa wanapata muda huo wakati wengine wamelala, hivyo kuna ambao wanachagua kuchelewa kulala na kuna ambao wanachagua kuwahi kuamka. Na wanachagua hayo kulingana na jinsi wao walivyo, yaani miili yao na mazingira yao.

Hadithi za mafanikio zinawapotosha wengi kwa sababu zinawaaminisha kwamba kama wakifanya kila ambacho waliofanikiwa walifanya, basi na wao watafanikiwa. Lakini huo siyo ukweli hata kidogo, hata hao waliofanikiwa, kama wangeanza upya leo na kurudia kufanya kila walichofanya kwa namna ile ile, bado hawatafanikiwa kama walivyofanikiwa awali.

Kumbuka kauli ya Thiel, kila wakati unatokea mara moja na hivyo kila wakati unahitaji mbinu zake.

Kwa hiyo tuachane kabisa na hadithi za mafanikio?

Baada ya kujua hili, unaweza kujiuliza kama Kocha anataka watu waachane kabisa na hadithi za mafanikio. Hilo siyo lengo langu, maana pia nimekuwa nakushirikisha hadithi mbalimbali za mafanikio.

Lengo langu ni wewe uzitumie hadithi za mafanikio kwa usahihi, uache kuangalia matokeo na uanze kuangalia chanzo.

Kwa kila hadithi ya mafanikio unayoisoma au kuisikia, angalia ni vitu gani vya tofauti ambavyo mtu alifanya, aliwezaje kuona fursa ambazo wengine hawazioni, aliwezaje kuvuka ugumu na changamoto za awali, aliwezaje kujiamini na kuwapuuza wale waliokuwa wanamkatisha tamaa.

Ukiweza kuyaona hayo kwa undani, utajifunza kitu kikubwa ambacho ukikiweka kwenye maisha yako kitakuwezesha kufanikiwa pia.

Kitu kingine kikubwa cha kufanya ni kutokuiga, haijalishi watu waliofanikiwa wamefanya nini, kamwe usiige, usijaribu kuwa mtu ambaye siye. Hakuna mtu amewahi kufanikiwa kwa kuiga au kuishi maisha yasiyo halisi kwake. Mafanikio ni magumu na yana changamoto nyingi, njia pekee ya kushinda ni kuwa wewe, maana huwezi kuchoka kuwa wewe.

Hivyo pamoja na kujifunza hadithi za waliofanikiwa, kabla hujafanyia kazi yale uliyojifunza, yatafakari maarifa uliyoyapata na jinsi wewe ulivyo.

Kabla hujasoma hadithi yoyote ile ya mafanikio lazima ujitambue wewe binafsi, ujue unataka nini kwenye haya maisha, kusudi lako ni nini, uimara wako na madhaifu yako ni yapi na utofauti gani ulionao na wengine.

Kwa kila hadithi ya mafanikio unayoisoma, tafakari maarifa unayoyapata na jiulize yanakusaidiaje kuwa bora zaidi kwa vile ulivyo sasa na siyo kukutaka ubadilike na kuwa mtu ambaye siyo halisi.

Usikubali kabisa kuishi maisha ya maigizo, hakuna ambaye amewahi kufikia mafanikio makubwa kwa kuiga, jitambue na kazana kuwa bora kwa namna ulivyo.

Karibu kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA upate vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu hivyo ambavyo vitakusaidia kuwa wewe ambaye ni bora zaidi na siyo kuishi kwa maigizo. Kujiunga na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania

Rafiki, karibu upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.