Mara nyingi watu wamekuwa wanashangaa nawezaje kukubaliana na kila mtu, hata kama anaamini na kusimamia kile ambacho ni tofauti kabisa na mimi.

Nina mifano mingi ya namna ambavyo watu wamekuwa wanashangazwa na hilo na hata wengine kukasirishwa.

Mfano tunaweza kuwa tunajadiliana jambo, ambapo niko upande fulani, halafu baada ya muda nikakubaliana na upande ambao nilikuwa napingana nao. Wale ambao waliona niko nao upande mmoja wananiona kama msaliti au niliyekosa msimamo.

Lakini huwa sijali, kwa sababu nilichojifunza na ambacho ninakiishi kwenye maisha yangu ni kukubali kutokukubaliana. Nimeona hii ni njia rahisi ya kuendesha maisha ambapo hutatengeneza changamoto zisizo na umuhimu.

Kwa kukubali kutokukubaliana, huwa nachukua nafasi ya kumsikiliza mtu na kumwelewa kwa nini yuko upande ambao yupo, na katika kusikiliza nikijifunza kitu ambacho sikuwa nakijua hapo awali, naweza kukubaliana naye.

Kwa njia hii naweza kujadiliana na mtu yeyote, bila ya kukwazika au kumwaza yeyote, kwa sababu sitegemei kila mtu aamini au awe na msimamo kama wangu na natoa muda kusikiliza na kujifunza.

Ukifanya mambo haya mawili; kuruhusu watu wawe tofauti na kusikiliza kujifunza badala ya kusikiliza kubisha, utakuwa na wakati tulivu sana kwenye maisha yako.

Lakini hili halimaanishi uwaruhusu watu wakudharau, kukudhihaki na kukulazimisha uwe au kufanya wanavyotaka wao. Hili halimaanishi kukosa msimamo kwenye maisha yako.

Msimamo lazima uwe nao, lakini uwe tayari kujifunza na kubadilika pale unapojua kitu bora ambacho hukuwa unajua.

Na muhimu zaidi, lazima uweke mipaka, kuna watu ambao ni wanazi, ambao hawafikiri kabisa badala yake wamepokea na kuamini kile wanachosimamia, hao ni hatari, kubaliana nao kuwaridhisha na endelea na mambo yako mengine.

Kujaribu kujadiliana na wanazi ni kupoteza muda wako, kwa sababu hawatajifunza chochote kutoka kwao na wewe hutajifunza chochote kutoka kwao. Mjadala wenye manufaa ni ule ambao kila mtu kuna kitu anajifunza, wanazi huwa hawajifunzi na hawafundishi, wanachohakikisha ni kusimamia kile walichonacho kwa gharama yoyote ile.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha