Kwenye maeneo mbalimbali yanayotoa huduma hasa za starehe, huwa yana taratibu zinazotofautiana za malipo. Kuna eneo ukienda unalipa kwanza ndiyo upewe huduma, wakati eneo jingine unapata huduma kwanza halafu unalipa mwisho. Kwa vyovyote vile huduma utapata, lakini lazima utalipia.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye maisha yetu, kuna gharama za kulipa kwenye haya maisha. Ila unachagua kama unataka kuzilipa sasa au utakuja kuzilipa baadaye. Hakuna anayeweza kuzikwepa gharama hizo, ni swala la muda tu, lakini lazima kila mtu azilipe.
Chukua mfano huu, kuna watu wawili wameanza wameajiriwa wakati mmoja, kipato chao kinalingana. Mmoja anaamua kuishi chini sana ya kipato chake, huku kiasi kikubwa akikiwekeza maeneo ambayo yanazalisha baadaye. Huyu anakuwa na maisha magumu mwanzoni. Wa pili anaamua kutumia kipato chake chote, hajibani, anajiambia anakula maisha, huyu anakuwa na maisha mazuri mwanzoni.
Wanaenda hivyo kwa miaka 20, wa kwanza anakuwa amefanya uwekezaji mkubwa unaomlipa vizuri na kuwa huru kutokufanya tena kazi, huku akiweza kuishi vile anavyotaka. Wa pili anakuwa amenasa kwenye madeni, akiwa hana uwekezaji wowote na anategemea kazi ndiyo apate pesa, siku kazi ikiisha hawezi tena kuendesha maisha.
Wote wamelipa gharama, wa kwanza amelipa mwanzoni na baadaye kuwa huru, wa pili ameanza kuwa huru na kuja kulipa gharama baadaye.
Kwa vyovyote vile, jua utalipa gharama fulani kwenye haya maisha, sasa ni wewe uchague kama utalipa mwanzoni au utakuja kulipa baadaye.
Chochote unachochagua kwenye maisha kuanzia mwenza wa kuishi naye, afya yako, eneo unaloishi, kazi na biashara unayofanya, uwekezaji unaofanya, marafiki unaokuwa nao na mengine, kuna gharama ya kulipa.
Ushauri wangu kwako ni huu, lipa gharama hizi mapema, usisubiri, maana unapokuja kulipa baadaye, unalipa kwa riba kubwa.
Jua gharama unazopaswa kulipa kwenye kila eneo la maisha yako, kisha anza kuzilipa mapema, usidanganyike kwamba kuna namna ya kukwepa gharama hizo, haipo. Anza kuzilipa sasa ili baadaye uwe huru.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Makala nzuri sana,kila mtu lazima alipe gharma fulani ktk maisha yake,mfano ni mimi mwenyewe nilichelewa kulipa gharama mwanzoni au sikulipa gharama sitahiki,sasa ndio napambana kuweka mambo sawa baada ya kupata Maarifa sahihi kupitia kisima cha Maarifa.asante sana kocha.
LikeLike
Vizuri Beatus, kwa kujua unalipa gharama, unakuwa na amani na kupambana kiusahihi.
LikeLike
Asante kocha nimeamua kuzipa sasa,sitaki kusubiria baadae nije kulipa kwa riba
LikeLike
Safi sana Kalenga.
LikeLike