Kikwazo kikubwa kinachowazuia watu kufanikiwa kwenye jambo lolote lile wanalofanya, ni kuanza kwa sababu zisizo sahihi.

Iwe ni kazi ambayo mtu amechagua kufanya au biashara, kuna sababu kuu mbili za mtu kuingia kwenye kitu hicho.

Sababu ya kwanza ni mtu kupenda kitu hicho kutoka ndani yake au kukichagua na kuwa tayari kuweka juhudi kuleta matokeo ya tofauti. Kwa sababu hii, mtu hasukumwi sana na kile anachotegemea kupata, bali anachokwenda kufanya.

Sababu ya pili ni wivu, mtu anaona wengine wamefanya kitu hicho na wakafanikiwa, na yeye anaona inabidi afanye kwa sababu anataka kufanikiwa. Kwenye sababu hii, mtu anasukumwa na nini anapata kuliko nini anakwenda kufanya.

Sehemu kubwa ya watu wanasukumwa kuingia kwenye kitu kwa wivu, kwa kuwa wamewaona wengine wanafanya na wamefanikiwa. Na hilo limepelekea wengi kushindwa.

Kwa sababu unapowaangalia watu kwa nje, kuna mengi ya ndani huyaoni. Unapoangalia mafanikio ya mtu, yanaonekana kama kitu rahisi, lakini ndani kuna magumu mengi amepambana nayo na anaendelea kupambana nayo, huwezi kuyaona.

Unapoingia kwenye kitu kwa sababu umeona mafanikio ya mtu ya nje na hukuona magumu, ukikutana na magumu unajiona huna bahati, na hapo safari inaisha.

Wewe angalia tu popote ulipo, ikianza biashara moja mpya na ikaonekana kufanikiwa, kila mtu anaanzisha biashara hiyo. Watu wakisikia kuna fursa mpya inalipa, kila mtu anaikimbilia. Mwishowe wengi wanashindwa na wachache walioingia kwa sababu wana msukumo wa ndani ndiyo wanaofanikiwa.

Chochote unachochagua kufanya, sikiliza msukumo wako wa ndani, angalia nini unakwenda kufanya kabla hujaangalia nini unakwenda kupata. Jua mafanikio yanayoonekana kwa nje ni tofauti kabisa na changamoto na magumu yaliyo ndani.

Na jua kabisa kwamba kabla hujafika kwenye mafanikio, kuna magumu mengi utayapitia.

Chagua kufanya kwa msukumo kutoka ndani na siyo kwa wivu kwa sababu wengine wamefanikiwa. Kufanya walichofanya wengine wakafanikiwa haikuhakikishii wewe kufanikiwa. Bali mafanikio yako yapo kwenye kile ulichochagua kufanya, kuweka thamani kubwa na kuzalisha matokeo ya tofauti.

Kila unapopata msukumo wa kuingia kwenye fursa mpya jiulize swali hili; je navutiwa na fursa hii kwa sababu nipo tayari kukabiliana na kila aina ya ugumu mpaka nifanikiwe au kwa sababu nimeona wengine wamefanikiwa? Kama jibu ni umejitoa kupambana, endelea na fanya hivyo. Ila kama jibu ni umeona wengine, acha.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha