Kwenye SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2020 mwanamafanikio mwenzetu Simeon Shimbe aliuliza; walimu wengi wa mambo ya fedha wanasisitiza zaidi mtu kuongeza kipato na siyo kupunguza matumizi, lakini kwenye kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA umesisitiza zaidi kupunguza matumizi, hiyo ikoje?
Nilimjibu ni kweli kuongeza kipato ni msingi muhimu mno kwenye kufikia uhuru wa kifedha, lakini kama hutadhibiti matumizi, kipato unachoongeza hutakiona.
Kwenye kitabu nimeeleza hili kwa kina, kwamba matumizi huwa yana tabia ya kuongezeka pale kipato kinapoongezeka. Na kila mtu ni shahidi kwenye hili, unapokuwa na kipato kidogo, matumizi yako yanakuwa yanaendana na kipato hicho. Lakini kipato kikiongezeka, ghafla matumizi nayo yanaongezeka.
Kwa kifupi, fedha ikiwepo huwa haikosi matumizi kabisa. Kuna kichekesho huwa kinazunguka mtandaoni kwamba ukishakuwa na fedha tu, matatizo ndiyo yanamiminika kwako, mara unasikia bibi yako kijijini kameza wembe, tuma chochote atibiwe. Ni kichekesho lakini kimebeba ujumbe mkubwa sana kuhusu fedha na matumizi, ukiwa nazo, matumizi huwa yanajitokeza, ambayo huwezi kuyakataa kwa sababu fedha unazo.
Hivyo ili kufikia uhuru wa kifedha, lazima ufanyie kazi yote mawili, kuongeza sana kipato chako na kudhibiti matumizi yako. Ukiongeza kipato bila kudhibiti matumizi ni sawa na kujaza maji ndoo iliyotoboka, utaweka maji mengi uwezavyo, lakini haitajaa.
Hivyo anza na yale matumizi ya msingi kwako, yale ambayo yanafanya maisha yako yaende vizuri, na hayo ndiyo unayohangaika nayo. Baada ya hapo kazana kuongeza sana kipato chako. Kwa kila kipato cha ziada unachopata, usikipeleke kwenye matumizi yoyote, bali kipeleke kwenye akiba na uwekezaji ili kizalishe zaidi.
Ukifanya hivyo kwa kipindi kifupi unajikuta umefika mbali kuliko kukazana kuongeza kipato tu huku matumizi nayo yakikua bila ya wewe kujua.
Dhibiti matumizi na kazana kuongeza kipato, haya mawili yanapaswa kwenda pamoja kama unataka kufikia uhuru wa kifedha.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Dhibiti matumizi na kazana kuongeza kipato.
Asante sana Kocha.
LikeLike
Karibu Datius
LikeLike