Watoto wadogo, huwa wanapelekwa kliniki kila mwezi ambapo pamoja na mambo mengine, wanaangaliwa ukuaji wao.
Ili kujua kama wanakua au la, kuna namba huwa zinafuatiliwa na kubwa kabisa ni uzito na urefu.
Huwezi kusema kama mtoto anakua au hakui kama huna namba hizo mbili na ndiyo maana huwa zinapimwa kila mwezi kwenye kliniki na mama kushauriwa kulingana na namba hizo.
Huo ni mfano mmoja, lakini unaonesha jinsi ambavyo namba zilivyo na umuhimu, kwenye kupima kitu chochote kile, namba zinahusika sana.
Kwenye kila eneo la maisha yako ambalo unataka kuliboresha, lazima uwe na namba. Kama unataka kujiboresha halafu huna namba, unajifurahisha.
Kwenye kila lengo unalojiwekea, lazima uwe na namba unazofanyia kazi, bila namba huwezi kujua hata pale unapolifikia lengo.
Ukijiambia unataka kupata pesa nyingi au kuwa tajiri mkubwa, unajidanganya, hakuna namna hapo, huwezi kujua kama unafikia lengo au la.
Ukijiambia unataka kupunguza uzito, wakati hujui uzito wako sasa na hujui unataka kuwa na uzito kiasi gani unajidanganya, huwezi kujua kama unafikia lengo.
Sasa kuna eneo moja ambalo linahitaji mno namba, lakini wengi wamekuwa wanapuuza.
Eneo hilo ni biashara, huwezi kuendesha biashara yenye mafanikio kama huna namba ambazo unazifuatilia kwa kina na usahihi kwenye biashara yako.
Zipo namba nyingi za kufuatilia, lakini za msingi kabisa ambazo nimekuwa nashauri kila anayefanya biashara azifuatilie ni MTAJI, MAUZO, WATEJA, GHARAMA na FAIDA.
Kama huzijui namba hizo kwa uhakika na ukawa unajipima nazo kila mwezi, huendeshi biashara, bali unacheza kamari.
Na kama ulifanikiwa kwenye biashara bila kujua namba hizo jua umebahatisha na unavyoendelea kwenda hivyo unakimbilia kwenye anguko.
Kazana vyovyote uwezavyo uweze kuwa na namba unazofuatilia kwenye biashara yako, ambazo unaweza kuzikokotoa kwa usahihi kila mwezi.
Kama ambavyo watoto wanahitaji kliniki ya kila mwezi kupima ukuaji wao, biashara pia inahitaji kliniki ya kila mwezi kupima ukuaji wake.
Chochote unachotaka kufikia au unachotaka kikue, kuwa na namba na ifuatilie kila mwezi, kila wiki au ikiwezekana kila siku.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,