Mafundisho mengi ya maendeleo binafsi, hamasa na mafanikio yamekuwa yanasisitiza sana mtu kuwa wewe.

Unaambiwa kuwa wewe, kwa sababu wengine wameshachukuliwa.

Unaambiwa ishi maisha yako kwa namna unavyochagua wewe, bila kujali wengine wanaishije au wanakuchukuliaje.

Unasisitizwa zaidi kutokufuata kundi, badala yake uende njia yako, ambayo ni ya kipekee kwako.

Ushauri huu ni mzuri mno, lakini haujakamilika, kwani ukifuatwa kichwa kichwa, utakuwa hatari mno.

Hebu fikiria kama umechagua kujipa raha muda wote, kupitia vilevi mbalimbali, hapo si umechagua kuwa wewe na kufanya yako? Je matokeo yatakuwaje?

Fikiria kama umejisikia kuperuzi mitandao ya kijamii siku nzima, maisha si yako na maamuzi ni yako? Je ni matokeo gani utayapata?

Vipi kama unatamani kufanya mapenzi na kila unayevutiwa naye, bila kujali kama uko kwenye mahusiano na mtu? Si ni maisha yako, umechagua kuyaishi utakavyo? Je maisha hayo yataendelea kuwaje?

Kwa mifano hii michache, utaona jinsi gani ushauri wa kuwa wewe, ishi utakavyo ulivyo hatari kama utakosa kiungo muhimu.

Hatari hiyo inaanzia kwa mtu mwenyewe, kwa kuathiri sana afya yake, kuharibu sifa yake na hata kukatisha uhai wake.

Lakini pia athari hiyo inakwenda kwa wengine, kwa kuanza na wale wa karibu, jamii na hata dunia kwa ujumla.

Japo unapaswa kuyaishi maisha yako, unapaswa kuyaishi kwa namna ambayo yana manufaa kwako na kwa wengine pia.

Swali ni je unawezaje kuyaishi maisha yako kwa namna hiyo?

Kitu kikuu kinachokosekana.

Ushauri wa kuwa wewe ni mzuri lakini umekosa kitu kimoja kikuu. Kitu hicho kikiwekwa kwenye ushauri huo, unakuwa ushauri mzuri mno na wenye manufaa kwa kila mtu.

Kitu kinachokosekana kwenye ushauri wa kuwa wewe ni UPENDO. Upendo ndiyo msingi mkuu wa maisha ambao ukisimamia, maisha yanakuwa bora kwa mtu na kwa wale wanaomzunguka.

Ukichagua kuongozwa na upendo kabla ya mengine yote, unapochagua kuwa wewe, unakuwa na manufaa makubwa kwako na kwa wengine pia.

Na upendo huu umegawanyika katika maeneo makuu matatu;

Moja ni upendo binafsi, kujipenda wewe mwenyewe. Lazima kwanza ujipende wewe mwenyewe. Ukijipenda mwenyewe, kwa kujikubali ulivyo, hutafanya chochote cha kukudhuru. Hutajiweka kwenye mazingira hatarishi na yanayokuathiri. Hutatumia vilevi kwa sababu unajua vinaharibu akili na mwili wako, hutajihusisha na mambo mabovu kwa sababu unajua hayana matokeo mazuri kwako.

Mbili ni kuwapenda wengine, wale wote wanaokuzunguka na unaokutana nao hata kutokukutana nao unawapenda. Unawapenda kweli kutoka ndani ya moyo wako na siyo kwa sababu kuna kitu unataka kutoka kwao. Unawakubali walivyo na siyo kuwataka wabadilike. Kwa kuwapenda wengine, hutafanya kitu ambacho kitawaumiza, hutawaibia, hutawasaliti, hutawatesa au kuwaumiza. Kila unachofanya kwa ajili ya wengine kinakuwa na manufaa kwao kwa sababu unawapenda.

Tatu ni kupenda kile unachofanya, shughuli yoyote unayochagua kufanya, iwe ni kazi au biashara, unaifanya kwa sababu unapenda kuifanya. Hata kama haikuwa ya ndoto yako, kwa sababu umechagua kuifanya, unaifanya kwa upendo wako wote. Hivyo mara zote unakuwa na hamasa kubwa ya kuifanya, hutafuti njia za kutoroka kuifanya na wala huifanyi hovyo hovyo.

Kama utaongozwa kwa nguvu kuu ya UPENDO, ni ruksa kuyaishi maisha yako, kuwa vile unavyotaka kuwa, kwa sababu chochote utakachofanya, kitakuwa bora kwako na kwa wengine, kwa sababu unajipenda na unawapenda.

Kama huongozwi na nguvu kuu ya upendo, ukichagua kuyaishi maisha yako utakuwa kiumbe hatari mno hapa duniani. Utafanya mambo ambayo yatakudhuru wewe mwenyewe na kuwadhuru wengine pia, utakuwa mbinafsi ambaye anaharibu kila anachokutana nacho na utapotea vibaya sana.

Jenga na ishi kwa msingi mkuu wa upendo na maisha yako yatakuwa bora kabisa, kwako na kwa wengine.

Kwenye KISIMA CHA MAARIFA, UPENDO ndiyo imani yetu kuu, ndiyo kitu ambacho kila mwanachama anakiamini na kukiishi kila siku. Kwa namna hii kila mmoja wetu anakuwa na maisha bora na kuwa huru kuyaishi maisha yake anavyotaka.

Unaweza kujifunza zaidi kuhusu nguvu ya upendo kwenye kukupa maisha huru na yenye furaha wakati wote kwa kusoma chambuzi za vitabu viwili vya mwandishi Don Miguel Ruiz vinavyoitwa THE FOUR AGREEMENTS na THE FIFTH AGREEMENT. Chambuzi za vitabu hivyo zinapatikana kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA, jiunge na usome kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania

Rafiki, karibu upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.