Kuna njia kuu mbili ambazo zimekuwa zinatumiwa na wengi kuingia kwenye biashara.
Njia ya kwanza ni mtu anapata wazo fulani la biashara, anaona ni wazo jipya ambalo halijawahi kufanyiwa kazi, anasukumwa kuanza kulifanyia kazi. Changamoto kubwa ya njia hii ni mara nyingi mawazo mapya huwa hayana soko, unaweza kuwa na kitu kizuri, lakini soko halikihitaji. Hivyo inakuwa vigumu kuanzisha na kukuza biashara kwa njia hii.
Njia ya pili ni kuanzia sokoni, kuona nini ambacho watu wanakihitaji, kisha kuwapatia. Wazo hili huwa linapata soko la uhakika, lakini huwa linakabiliana na ushindani mkali kwa sababu soko unaliona wewe kila mtu pia analiona. Na kama umesukumwa kuingia kwa sababu soko lipo tu, utakachokuwa unaangalia ni faida tu na hivyo hutafanya vitu vya tofauti vinavyokukinga na ushindani.
Kuna njia ya tatu ambayo ukiitumia unapata manufaa ya njia hizo mbili za kwanza na kuepuka changamoto zake. Ni njia yenye nguvu kubwa ukiweza kuitumia vizuri.
Njia hiyo ni kuanzia ndani yako, kisha kwenda sokoni na ndipo kuanza biashara.
Unaanzia ndani yako kwa kuangalia nini hasa unapenda kufanya, kipi unaweza kukifanya tofauti kabisa na wengine wanavyoweza kufanya. Kipi ukigusa kila mtu anakusifia, kwa kukuambia uko vizuri kwenye kitu hicho. Kinaweza kuwa kimoja au vingi, muhimu ni kuwe na msukumo mkubwa ndani yako kwenye kitu hicho.
Unaenda sokoni kwa kuangalia mahitaji makubwa ambayo watu wanayo, orodhesha yote ambayo wale wanaokuzunguka wanasumbuka nayo na hawajapata jawabu la uhakika.
Unaanza biashara kwa kuoanisha kile kinachotoka ndani yako na hitaji lililopo sokoni. Biashara hii inakuwa na nguvu kwa sababu msukumo wa kufanya unatoka ndani yako hivyo utajituma sana lakini pia soko lipo hivyo utaweza kunufaika.
Njia hii inaondoa changamoto ya wazo zuri kukosa soko na ya ushindani, kwa sababu unapokuwa na msukumo wa ndani, unaweza kujitofautisha kwa namna ambayo hakuna mshindani anayeweza kukuondoa sokoni.
Tumia njia hii ya tatu kwenye kuanzisha na hata kuboresha biashara unayofanya sasa na utaweza kupiga hatua kubwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Ahsante Sana kocha nimekuelewa vyema.
LikeLike
Karibu.
LikeLike
Shukrani sana Kocha kwa makala hii nzuri.
LikeLike