Kamwe usifanye maamuzi ukiwa kwenye hali hizo nne. Kwani maamuzi utakayoyafanya ukiwa kwenye hali hizo, huishia kuwa maamuzi mabovu na yatakayokugharimu mno. Hali hizo huwa zinaondoa kabisa uwezo wa akili kufikiri kwa umakini na kufikia maamuzi sahihi. Unapofanya maamuzi kwenye hali hizo, unakuwa umesukumwa zaidi na hisia kuliko kufikiri. Kila unapojigundua upo kwenye hali hizo, epuka kabisa kufanya maamuzi, hata kama unalazimishwa kiasi gani, hata kama unaambiwa usipofanya maamuzi hapo unakosa. Kwa sababu wapo watu wanaokuweka kwenye hali hizo kwa makusudi ili ufanye maamuzi yatakayowanufaisha. Mfano mtu anakukasirisha kwa makusudi, ili ufanye maamuzi mabovu yatakayokuumiza wewe na kumnufaisha yeye. Kadhalika kwa hali nyingine, wapo watu wanaoweza kuzitumia kupata wanachotaka. Ufanye nini? Unapojikuta upo kwenye hali hizo nne, kuna mengi unayoweza kufanya yatakayosaidia kuondokana na hali hizo. Kama ni njaa pata chakula, na hapo hakikisha unapata chakula sahihi na kwa kiwango cha kawaida, usikimbilie kupata chakula kingi, kwani ukishiba sana pia itaathiri ufanyaji wako wa mazoezi. Unapokuwa na uchovu pumzika, jiwekee sera yako binafsi kwamba maamuzi yote muhimu kwako unayafanya mwanzo wa siku yako, kabla hujachoka. Na kama kuna maamuzi inabidi ufanye kwenye mwisho wa siku, mfano una mkutano unafanyika jioni, basi mchana tenga muda wa kupumzika na unapotoka kwenye mapumziko ndiyo uende kwenye maamuzi hayo. Bingwa mmoja wa mchezo wa chess alikuwa na tabia ya kulala kabla ya kila pambano kubwa, hivyo aliingia kwenye pambano akiwa hana uchovu. Unapokuwa na hasira fanya kitu kinachokuondoa kwenye kufikiria kile kinachokusairisha, inaweza kuwa kujiandikia barua au kuandika chochote unachoshukuru kuwa nacho kwenye maisha yako. Unaweza pia kuwa na mazungumzo na mtu ambaye mtajadili kitu cha tofauti kabisa. Unapokuwa na upweke, fanya kitu cha kukuondoa eneo moja ambalo unakuwa umekaa kwa muda mrefu. Unaweza kufanya matembezi kwenye eneo la asili na hapo ukajikuta umemezwa na asili kiasi cha kujiona haupo peke yako. Pia unaweza kutafuta wa kufanya naye mazungumzo. Kwa vyovyote vile, usifanye maamuzi muhimu ukiwa kwenye hali hizo nne na ukishajigundua upo kwenye hali yoyote kati ya hizo, chukua hatua ya kuondokana nayo kama tulivyojifunza hapa. Kila la Kheri Rafiki Yangu. Rafiki na Kocha wako, Dr. Makirita Amani, www.amkamtanzania.com/kocha