Kila mmoja wetu ana ndoto kubwa ya maisha yake, kitu ambacho anataka kuwa au kufikia kwenye maisha hayo. Ndoto ndiyo kitu kinachomsukuma mtu kufanya kile anachofanya.

Kwenye maisha, wale wanaoishi na kufikia ndoto zao huwa wanafanikiwa na kuwa na furaha kuliko wanaofanikiwa kwa kutokuishi na kufikia ndoto zao.

Lakini wote tunajua jinsi maisha yalivyo, mipango siyo matumizi, unapanga hilo na yaliyo nje ya uwezo wako yanakuwa kikwazo kwako kufikia ndoto yako.

Watu wengi wamefika kwenye hali kama hii, ya nguvu za nje kuwa kikwazo kufikia ndoto zao na wasijue wafanye nini. Wapo ambao wanaamua kuachana na ndoto hizo, lakini baadaye wanajutia. Na wapo wanaopambana kwa kila namna kuzifikia, lakini wanajikuta wamepoteza muda na hata walipofikia ndoto haijawa kama walivyotegemea.

Je ni hatua gani sahihi kuchukua unapojikuta kwenye njia panda ya aina hii? Huo ndiyo ushauri tunaokwenda kuupata kwenye makala ya leo ya ushauri wa changamoto zinazotuzuia kufikia mafanikio makubwa.

Msomaji mwenzetu Sprian alituandikia kuhusu hili la njia panda kwenye ndoto akiomba ushauri, karibu usome alichoandika na kisha kusoma ushauri wa hatua sahihi za kuchukua.

Naitwa Sprian G. C, naishi Sumbawanga vijijini. Nina umri wa miaka 28. Katika maisha yangu yote nilipenda na bado napenda nije niwe askari, lakini kwa bahati mbaya nilikatisha masomo nikiwa kidato cha pili, na huu ni mwaka wa 8 tangu niache masomo baada ya wazazi kukosa fedha ya kuniendeleza kimasomo. Lakini baada ya kuacha masomo nilijiwekea lengo la kutafuta pesa ili nije nijiendeleze kimasomo. Sasa nina mtaji wa milioni 30 niliyoipata kwa njia ya kilimo na biashara ya mazao. Sasa nimeona ni muda muafaka wa kwenda shule, ili nije nitimize ndoto yangu ya kuwa askari. Changamoto yangu kubwa ni hii ‘Napenda sana nije niwe askari na ninahisi naweza kupata matatizo ya akili nisipotimiza ndoto hii kutokana na jinsi ninavyoipenda. Lakini kwa bahati mbaya sina uhakika 100% kama nitakuja kupata ufaulu mzuri katika masomo yangu na pia sina uhakika wa kuja kupata ajira ya hiyo kazi ninayoipenda. Tafadhali naomba mchango wenu wa mawazo katika hili.

Kwako rafiki yangu Sprian,

Umeeleza vizuri ndoto kubwa uliyonayo na changamoto ambazo umekutana nazo na zikawa kikwazo kikubwa kwak.

Umeeleza vizuri njia panda uliyopo,  kwamba usipotimiza ndoto hiyo unaweza kuchanganyikiwa kabisa. Lakini pia ukiitimiza huna uhakika kama utapata fursa nzuri kwenye hilo.

Swali ni ufanye nini kuondoka kwenye mkwamo uliopo sasa?

Kwa kuzingatia hali uliyonayo sasa, kuanzia umri na kipato, ushauri wangu kwako ni uchukue njia ya tofauti ambayo ni kutimiza ndoto yako kwa njia mbadala.

Ukiachana na ndoto yako kabisa hatakuwa na maisha tulivu, hata apate mafanikio kiasi gani, bado ndoto ya kuwa askari itakuwa inakuandama na hapo utaona maisha yako hayajakamilika.

Lakini pia ukitimiza ndoto hiyo, kwa kurudi shuleni na kuanza tena kusoma, mpaka uje ufikie kiwango hicho cha uaskari kuna mengi yaliyo nje ya uwezo wako ambayo yanaweza kuwa kikwazo kikubwa kwako. Kama ulivyoainisha, ufaulu na nafasi za ajira ni vitu ambavyo mtu huwezi kuwa na uhakika navyo.

Hivyo hatua ya kuchukua hapo ni kutimiza ndoto ya kuwa askari kwa njia mbadala.

Hapo anza kwa kujiuliza sababu hasa ya wewe kutaka kuwa askari, nini kinakusukuma wewe uwe askari?

Naamini siyo kuvaa yale mavazi ya askari ndiyo kinakusukuma, lazima kutakuwa na kitu cha ndani kabisa kuhusu uaskari ambacho kimekuvutia.

Na kama utachimba ndani, utajionea wazi kwamba ile huduma ambayo nafasi ya uaskari inakupa kutoa kwenye jamii ndiyo inayokusukuma wewe kuwa askari.

Inaweza kuwa kuwalinda watu au kuwasaidia wale wanaokosa haki au kunyanyaswa na wengine. Huenda kuna hali wewe au watu wa karibu wamewahi kupitia ambayo ilikufanya ujiambie nikiwa askari sitaruhusu hali kama hii itokee kwa wengine.

Hivyo chimba ndani yako kujua msukumo hasa unatoka wapi.

Ukishajua msukumo wako ni upi, angalia njia mbadala za kukuwezesha kutimiza hilo.

Zipo fursa nyingi unazoweza kutumia kutimiza ule msukumo wako wa ndani ukishaujua.

Mfano kama msukumo ilikuwa kuwapa watu ulinzi, unaweza kuanzisha kampuni binafsi ya ulinzi ambayo itakuwezesha kufikia ndoto hiyo. Ukawaajiri wale wenye fani ya uaskari, ukawapa ndoto uliyonayo na kwa pamoja mkaifikia.

Kama ni kuondoa uonevu zipo njia mbalimbali unazoweza kutumia kufikia hilo.

Mambo ya kuzingatia wakati unatimiza ndoto kwa njia mbadala.

Ukishaamua kutimiza ndoto yako kwa njia mbadala, sasa jiweke kwenye njia ambayo hakuna kikwazo kingine kitakachokuzuia.

Kitu cha kwanza ni kujijengea uhuru wa kipato.

Hilo umeshaanza kulifanya kwa kuweza kutengeneza mtaji huo wa milioni 30 kupitia kilimo. Endelea kutengeneza kipato zaidi kwa fursa zinazokuzunguka na kufanya uwekezaji ambao utakuingizia kipato kitakachokuweka huru baadaye.

Njia ulizoweza kutumia kuzalisha fedha ulizonazo sasa, zitumie kwa ubora zaidi ili uzalishe kipato zaidi.

Kupitia kilimo fanya kwa njia bora na kwa ukubwa zaidi ili uweze kukuza kipato chako.

Pia tengeneza njia nyingine za kuingiza kipato kama biashara na uwekezaji ili uweze kufikia uhuru wa kifedha.

Kitu cha pili ni kujiendeleza kielimu.

Pamoja na kwamba hutasomea uaskari moja kwa moja, unaweza kujiendeleza kielimu kwa lengo la kupata ufahamu zaidi utakaokusaidia kwenye shughuli unazofanya na hata kwenye njia mbadala ya kufikia ndoto ya uaskari itakayokuwa umechagua.

Unapojiendeleza kielimu sasa hufanyi kwa sababu unataka ufaulu na uajiriwe, bali unafanya hivyo kwa sababu unataka kujua zaidi na kutumia ujuzi huo kutimiza vizuri malengo yako.

Kitu cha tatu ni kuanza kidogo kidogo kutimiza ndoto yako.

Kwa njia mbadala unayotumia kufikia ndoto yako, anza kidogo kidogo. Anza kwa kufanya utafiti wa namna bora ya kutekeleza. Angalia wale ambao wanatekeleza sasa na jifunze kwao jinsi wanavyofanya kwa njia hiyo utajifunza mengi.

Baada ya kujifunza chagua hatua ndogo kabisa unazoweza kuanza nazo huku ukijua itakuhitaji muda mpaka kufikia ndoto hiyo kwa ukamilifu wake.

Kwa kuzingatia haya uliyojifunza hapa, utaweza kufikia ndoto yako ua uaskari kwa njia mbadala, kwa kupata fursa ya kutimiza haja ya moyo wako hata kama hutakuwa askari moja kwa moja.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania

Rafiki, karibu upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp