“If you make it a habit not to blame others, you will feel the growth of the ability to love in your soul, and you will see the growth of goodness in your life.” — Leo Tolstoy

Kulaumu wengine kwa yale yanayoendelea kwenye maisha yako ni kitu rahisi na unachopenda na kufurahia kufanya.
Pale mambo yanapokwenda tofauti na ulivyotegemea, ni rahisi kuangalia nani aliyesababisha na kisha kumlaumu.
Utajisikia vizuri baada ya kulaumu, kwa kuona kosa siyo lako.
Lakini lawama hizo hazitakuwa na manufaa kwako, maana hazitabadili matokeo uliyopata.
Utaendelea kubaki pale ulipo na hutajifunza unapokosea na kuweza kuchukua hatua sahihi.

Kama unataka kupiga hatua kwenye maisha yako, ni lazima uache mara moja tabia ya kulaumu wengine.
Kwa matokeo yoyote unayopata au hali yoyote unayopitia, wewe mwenyewe ndiye uliyechangia kwa kiasi kikubwa.
Hata kama kuna mwingine amesababisha, bado ni wewe umempa nafasi na ruhusa ya kufanya hivyo.
Ukijua hilo, utaweza kuchukua hatua sahihi.

Kuacha tabia ya kulalamika kuna manufaa mengine mawili;
Kunakuwezesha kuwa na upendo zaidi, kwako na kwa wengine. Huwezi kuwa na upendo kama unalaumu.
Pia kunakuza wema ndani yako, kwa kutokulaumu, unakuwa mwema.

Achana kabisa na tabia ya kulaumu, ni kitu tulichozoea kufanya na ambacho ni rahisi, kitu ambacho waliokuzunguka wanafanya mara kwa mara, hivyo lazima uwe makini sana kukiepuka.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu bila ukinzani, soma hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/12/10/2171

Rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani.