Kuna sumu ambazo ukitumia unadhurika mara moja, yaani matokeo yake ni ya papo kwa hapo.
Halafu kuna sumu ambazo huwa madhara yake ni ya muda mrefu, yaani matokeo yake yanahitaji muda mpaka yaanze kuonekana.
Huwa tunahofia zaidi sumu za matokeo ya haraka kuliko za matokeo ya muda mrefu. Lakini kama tunataka kuwa na maisha mazuri, tunapaswa kuzihofia zaidi sumu za muda mrefu.
Sumu za madhara ya muda mfupi unaweza kuchukua hatua haraka na kuondoa madhara yake kabla hayajawa na hatari kubwa.
Lakini sumu za madhara ya muda mrefu huwezi kuchukua hatua haraka, kwa sababu madhara hayaonekani. Mpaka unapokuja kustuka na kutaka kuchukua hatua, unakuwa umeshachelewa na madhara ni makubwa.
Kuna sumu za aina hii ambazo unapaswa kuwa makini nazo kwenye maeneo mbalimbali ya maisha yako.
Eneo la kwanza ni afya yako ya mwili, kuna vitu unakula ambavyo madhara yake huyaoni haraka, ila baadaye vinakuletea madhara makubwa. Vyakula vya wanga sana na vilevi unaweza kuvifurahia sasa, lakini kadiri muda unavyokwenda vinakuwa na madhara makubwa kwenye afya yako. Jitahadhari na kila kitu kabla hujakiingiza kwenye mwili wako.
Eneo la pili ni fikra zako, hizi ndiyo unapaswa kuwa nazo makini kwani kuna watu wanakupandikizia fikra fulani ambazo madhara yake hutayaona sasa. Kila fikra unayokuwa nayo inachangia namna maisha yako yatakuwa. Unapokuwa na fikra nyingi zisizo sahihi, maisha yako yanakuwa siyo sahihi pia.
Eneo la tatu ni kwenye fedha, kuna vitu unafanya kwenye eneo lako la fedha sasa na usione madhara yake, lakini baadaye vitakuwa mzigo kwako. Vikubwa kabisa ni matumizi ya kipato chako na kukopa. Kama hudhibiti matumizi yako kipato kikiwa kidogo, kitakapokua matatizo yatakuwa makubwa zaidi. Na kama una tabia ya kukopa, utatatua shida za sasa, ila utatengeneza kubwa zaidi kwa baadaye.
Eneo la nne ni mahusiano, kuna mambo unaweza kufanya yasiwe na madhara makubwa sasa, ila yakaweka ufa kwenye mahusiano yako na baadaye yakapelekea mahusiano hayo kuvunjika. Mfano ni kuvunja uaminifu kwenye vitu vidogo vidogo.
Eneo la tano ni shughuli unazofanya, yaani kazi au biashara, kuna vitu vidogo vidogo unaweza kuwa unafanya au kutokufanya kwenye shughuli zako na usione madhara yake sasa ila baadaye. Moja ya vitu hivyo ni umakini na kujali, kutokujali na kutokuweka umakini kwenye kile unachofanya ni chanzo cha mtu kuishia kuwa hovyo kwenye kazi au biashara anayofanya.
Kila unachotaka kufanya, jipe sekunde chache kutafakari matokeo yake ya baadaye, kama ni sumu inayoua taratibu, jiepushe nayo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Hakika aya ni maeneo matano muhimu tunayopaswa kuyaelewa vizuri ili tuweze kujiepusha na sumu ndogo ndogo zinazoweza kuyaharibu na kutuletea matatizo makubwa kwenye maisha yetu.
Ubarikiwe sana Kocha kwa makala hii.
LikeLike
Karibu.
LikeLike
Makala bora sana ya mwaka
LikeLike
Karibu Nyamizi.
LikeLike