Kulala masikini na kuamka tajiri au ‘zali la mentali’ ni mtazamo ambao wengi wamekuwa nao kuhusu mafanikio na umekuwa unawaangusha.

Kwa mtazamo huo, watu huamini kwamba ipo njia ya mkato ya wao kufika kwenye mafanikio makubwa. Kwa kuamini hivyo, hupoteza muda mwingi kuitafuta na hawaipati.

Kilicho kibaya zaidi ni kwamba katika kutafuta huko, hulaghaiwa na njia za kitapeli, wakiamini wanakwenda kupata mafanikio lakini wanaishia kutapeliwa.

Watu wote wanaotapeliwa huwa wanaamini kwenye njia ya mkato ya kufanikiwa. Wale ambao hawaamini kwenye njia hiyo, wale ambao wanajua mafanikio ya aina yoyote ile yanahitaji muda na kazi, huwa hawatapeliki, kwa sababu hawana hata muda wa kuwasikiliza wale wanaokuja kwao na utapeli.

Kila siku watu wamekuwa wanatapeliwa na kulizwa na njia mbalimbali za mkato za kupata utajiri na mafanikio makubwa. Lakini njia hizo zina madhaifu ya wazi kabisa, ambayo mtu akiwa makini anaweza kuyaona na akaepuka kutapeliwa.

Kwenye makala ya leo, tunakwenda kujadili kwa kina vipindi vinne vya ukuaji kwenye safari ya maisha yako ya mafanikio. Kwa kuvijua vipindi hivi na kuvifanyia kazi, siyo tu utaepuka kutapeliwa, bali pia utaweza kujipanga vizuri na kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako.

Kipindi cha kwanza; kujifunza (miaka 3).

Kitu chochote unachoanza kufanya, unakuwa hukijui kwa undani. Hata kama umekisomea na kuhitimu, ukasoma vitabu, ukasikiliza hadithi za waliofanikiwa kwenye kitu hicho, bado hukijui kwa undani.

Ni mpaka unapoanza kufanya kitu hicho ndiyo unajua hujui, unapoingia ndani ndiyo unajua ni kwa uchache kiasi gani unajua kitu hicho.

Hivyo miaka mitatu ya mwanzo ni ya kujifunza, ni miaka ya kukijua kitu kiundani na kujua jinsi unavyopaswa kukifanya.

Hii inakuwa miaka ya kujaribu na kushindwa, miaka ya kupata hasara na kupoteza muda, nguvu na fedha kwenye mambo ambayo matokeo yake hutayaona haraka.

Lakini yote unayoweka na huoni matokeo yake sasa hayajapotea, bali ni uwekezaji ambao baadaye utakulipa sana.

Miaka mitatu ya kwanza ambayo unajifunza hutatengeneza kipato chochote, kama ni biashara, hakuna faida yoyote utakayokuwa unatengeneza, hasa ukilinganisha na uwekezaji ambao unakuwa unaufanya.

Hiki ni kipindi ambacho unahitaji uvumilivu wa hali ya juu na kuamua kweli hicho ndiyo kitu unachotaka kwenye maisha yako. Maana kama siyo unachotaka kweli, hutaweza kukivumilia kwa miaka mitatu.

Kipindi cha pili; kuanza kuingiza kipato (miaka 2).

Baada ya kukijua kwa undani kile unachofanya, unafika hatua ya kuweza kuingiza kipato kupitia kitu hicho. Hapo unakuwa umeingia kwenye kipindi cha pili ambacho kinachukua miaka miwili.

Katika kipindi hiki unaingiza kipato, lakini siyo kikubwa sana. Ni kipato kidogo ukilinganisha na uwekezaji ambao umeufanya kwenye kitu hicho.

Lakini ni kipindi ambacho kinakupa faraja kwamba uwekezaji uliofanya haujapotea na kama ukiendelea basi utaweza kufanya makubwa zaidi.

Kwenye biashara hiki ni kipindi ambacho unatengeneza faida, ila bado unahitaji kuweka kazi na kuendelea kuwekeza kwenye biashara hiyo.

Hiki ni kipindi ambacho unapaswa kuwa na tahadhari usijisahau. Wengi wanapofika hatua hii hujisahau kwa kuridhika haraka na kinachotokea ni wanaanguka kabisa.

Kipindi cha tatu; kutengeneza kipato cha uhakika (miaka 4).

Baada ya kuanza kuingiza kipato na kupata matumaini ya kuendelea kuweka juhudi na kuwekeza, unafika kipindi cha tatu ambacho ni kutengeneza kipati cha uhakika.

Kipindi hiki huchukua miaka mingine minne, ambapo mtu anakuwa amefanya uwekezaji zaidi kwenye yale maeneo ambayo aliona fursa za kutengeneza kipato zaidi.

Katika kipindi hiki, mtu anakuwa na kipato cha uhakika cha kumwezesha kuendesha maisha yake bila ya shida yoyote ile.

Katika kipindi hiki mtu anakuwa huru, japo siyo moja kwa moja, kwani kile anachokifanya bado kinakuwa kinahitaji maamuzi yake kwenye nyakati muhimu.

Kwa biashara hiki ni kipindi ambapo biashara inaweza kujiendesha hata kama mwanzilishi wake hayupo, lakini bado yeye ndiye mfanyaji wa maamuzi yote muhimu ya biashara.

Hiki ni kipindi ambacho unapaswa kuwa mnyenyekevu kwa sababu hatua unazokuwa umepiga zinaweza kukupa kiburi na kufanya uone unaweza kila kitu. Hapa watu hushawishika kwenda kuanza vitu vingine wakidhani uzoefu walioupata kwenye kile walichofikisha hapo utawasaidia kwenye chochote watakachofanya.

Kipindi cha nne;  kufikia mafanikio makubwa (miaka 6).

Mafanikio makubwa kabisa ndiyo hatua ya juu ya safari ya mafanikio. Hapa ni pale ambapo mtu unakuwa umepata uhuru wako kamili kutoka kwenye kile unachofanya.

Kitu hicho kinaweza kwenda chenyewe hata kama wewe haupo kabisa. Hata maamuzi muhimu kabisa hayakutegemei wewe.

Hiki ni kipindi cha nne cha safari ya mafanikio ambacho huchukua mpaka miaka 6 kukifikia. Katika kipindi hiki, mtu anakuwa na uhakika wa kudumu kwenye mafanikio yake milele.

Hiki ni kipindi unachopaswa kuwa makini usilete madhara kwenye maisha ya wengine na dunia kwa ujumla. Wengi katika kipindi hiki wanakuwa na nguvu na mamlaka makubwa ambayo wasipokuwa na tahadhari wanaweza kuharibu maisha ya wengine na hata kuleta madhara kwa dunia nzima. Ni kipindi cha kuacha kujiangalia na kuwaangalia wengine zaidi.

Hitaji kuu; ung’ang’anizi.

Ukijumlisha hiyo miaka hapo juu, unapata ni miaka 9 mpaka kutengeneza kipato cha uhakika na miaka 15 mpaka kufika mafanikio ya juu kabisa.

Kwa kifupi ni inahitaji muda, siyo kitu cha haraka.

Hivyo chochote unachofanya au unachotaka kuanza kufanya, kama hujioni ukiendelea kukifanya kwa miaka 10 mpaka 15 ijayo, achana nacho, unapoteza muda wako, hutaweza kupata mafanikio makubwa kupitia kitu hicho.

Lazima uwe tayari kung’ang’ana kweli kweli ili kufika kwenye mafanikio makubwa.

Lazima uwe umechagua kweli kutoka ndani yako na kuwa tayari kukabiliana na kila ugumu utakaokutana nao kwenye safari yako.

Lazima uingie kwenye kitu ukijiambia hiki ndiyo nakwenda kukifanya kwenye maisha yangu na siyo unachokwenda kujaribu.

Kama bado ulikuwa hujafanya uchaguzi sahihi wa maisha yako wa nini unataka na nini unakwenda kufanya, ufanye sasa kwa kutumia vipindi hivi vinne.

Na kama tayari ulishajua nini unataka na nini unafanya, basi jua uko kwenye hatua ipi na jua hatua zilizo mbele yako, kisha jiandae kuzikabili ili uweze kufanikiwa sana.

Vitabu vya kusoma.

Safari ya mafanikio ni ya muda mrefu, kama tulivyojifunza hapo, kuna vipindi vinne ambavyo vina changamoto mbalimbali.

Kujifunza ni moja ya hitaji muhimu kwenye safari yako ya mafanikio.

Vifuatavyo ni vitabu muhimu sana vitakavyokusaidia kwenye safari hii ya mafanikio, hakikisha unavisoma na kuchukua hatua kwa yale unayojifunza.

1. ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, kitabu hiki kinakupa misingi sahihi ya kifedha itakayokuwezesha kufika kwenye utajiri na uhuru wa kifedha.

2. ELIMU YA MSINGI YA BIASHARA, kitabu hiki kinakupa maarifa ya kibiashara ambayo ni mwongozo wa kufanikiwa kwenye biashara.

3. UNA NGUVU YA KUTENDA MIUJIZA, kwa kuangalia urefu wa safari ya mafanikio unaweza kufikiri haiwezekani, ila inawezekana sana kwa sababu ndani yako una nguvu kubwa ya kutenda miujiza. Kitabu hiki kitakuonesha nguvu hiyo na jinsi unavyoweza kuitumia.

Kupata vitabu hivyo, wasiliana na 0752 977 170 na utatumiwa au kuletewa vitabu ulipo.

Rafiki, karibu upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania