Watu hawawezi kununua kitu unachouza kama hawajahamasika,
Na huwezi kuwahamasisha watu kununua kitu kama wewe mwenyewe hujahamasika,
Na zaidi, huwezi kuhamasika kama hujakikubali kweli kile unachouza.
Hivyo kama unataka kuuza vizuri kitu, kinunue wewe mwenyewe kwanza, kikubali kweli kweli, hamasika juu ya kitu hicho.
Kadiri unavyokuwa umehamasika kuhusu kitu, ndivyo na wengine nao wanavyohamasika kupitia wewe.
Ndiyo maana inashauriwa sana kuuza kitu ambacho wewe mwenyewe unaweza kukitumia au unaweza kumnunulia mtu wako wa karibu kukitumia. Wewe mwenyewe unapaswa kuwa mteja wa kwanza wa kile unachouza, na hapo utaweza kumshawishi mwenye uhitaji kukinunua.
Uzuri wa wewe kuwa mteja wa unachouza, ni kwamba mtu anapokuja kwako na mapingamizi, unaweza kuyapangua vizuri. Mtu anaweza kukuambia hiyo ni ghali sana, naweza kupata rahisi sehemu nyingine. Kwa kuwa wewe ni mtumiaji, utakuwa umejaribu aina tofauti na kujua madhara yake, hivyo utamshirikisha uzoefu wako.
Kadhalika wale wanaokuambia haifanyi kazi kama unavyoeleza, utawapa mfano wako mwenyewe na hakuna anayeweza kupingana na mfano hai wa kitu.
Ukishakuwa mteja wa kile unachouza, kinachofuata ni kuwalenga wale wenye uhitaji kama ambao wewe umekuwa nao mpaka kuwa tayari kununua kitu hicho na kisha kuwaonesha ni kwa nini wanunue kwako na sasa.
Hakuna mtu anayeamka asubuhi na kujiambia leo naenda kununua kitu fulani ili nimfaidishe muuzaji, kila mtu anaamka akiwa na uhitaji au changamoto anayotaka kuitatua, kwa gharama nafuu kwake.
Wewe ukiweza kuwaonesha wale uliowachagua kwamba unaweza kuwatatulia changamoto zao au kutatua matatizo yao na kwa gharama rahisi, watakuwa tayari kununua kwako.
Pia ukishakuwa mteja wa unachouza, ni rahisi kuongeza thamani zaidi na hivyo kuwavutia wateja kununua zaidi. Kadiri unavyoweza thamani kwenye kile unachouza ndivyo unavyoweza kuwashawishi wengi zaidi kununua.
Nunua kabla hujauza na utaweza kuuza kwa wengi zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,