Ni lazima uweze kutofautisha maoni na ukweli ili uweze kufanya maamuzi sahihi.

Watu wengi wanafanya makosa kwa kuchukulia maoni kama ukweli na hivyo kufanya maamuzi ambayo ni mabovu.

Ukweli ni ukweli, haubadiliki kulingana na eneo, mtu au hali.

Maoni ni mtazamo wa mtu au watu, ambayo huwa yanabadilika kulingana na eneo, hali na watu.

Kwa zama tunazoishi sasa, kila mtu ana uwanja wa kushirikisha maoni yake na wapo ambao wana kelele na ushawishi mkubwa, ambao wakitoa maoni yao unaweza kufikiri ndiyo ukweli.

Wajibu wako ni kuweza kuchambua maoni na ukweli.

Chochote ambacho inabidi ushawishiwe sana na ambacho inabidi kitetewe sana ni maoni.

Ukweli huwa hauhitaji kulazimishwa, wala hauhitaji kutetewa sana. Ukweli unasimama kama ukweli na hauyumbishwi na chochote.

Karibu kila kitu ambacho wengine wanakuambia na kukushauri au kukushawishi ni maoni yao binafsi. Na ukitaka kuthibitisha hilo, utaona kuna wengine ambao wanakushawishi kilicho kinyume kabisa na hicho. Na vyote viwili ambavyo vinapingana, vinafanya kazi.

Watu wenye misimamo mikali huwa wanajisahau, wanafikiri maoni yao ndiyo ukweli na kila mtu anapaswa kuyafuata na kuyaishi. Lakini huo siyo ukweli, haijalishi mtu anayaamini maoni yake kiasi gani, hayatageuka kuwa ukweli.

Kama maoni yangekuwa sheria, tungeshakufa wote duniani. Hebu fikiri ni mara ngapi mtu amekuudhi na ukatamani hata angekufa. Hayo yalikuwa maoni tu na yalichochewa na hasira. Kama kila maoni yangetekelezwa, dunia ingekuwa haina yeyote.

Unapofanya maamuzi, angalia ukweli. Sikiliza maoni utakavyo, lakini msingi wako unapaswa kuwa kwenye ukweli. Kwa sababu maoni yanabadilika, ukifanya maamuzi leo kwa maoni ya leo, kesho maoni yatabadilika na utaona uamuzi uliofanya siyo sahihi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha