“There are more things likely to frighten us than there are to crush us; we suffer more often in imagination than in reality.” – Seneca

Maisha tayari ni magumu, ila huwa tunazidisha ugumu huo kwa mambo tunayoyafanya.
Moja ya mambo tunayofanya na kupelekea maisha kuwa magumu na kujitesa zaidi ni kuhofia.

Mambo mengi unayohofia huwa hayatokei na hata yakitokea siyo kwa kiwango ambacho tulikuwa tunahofia.
Hofu huwa ni zao la kufikiria mambo ambayo bado hujayafikia.
Ni sawa na kutabiri nini kitatokea siku zijazo.
Lakini kitu kimoja ambacho tuna uhakika nacho ni hakuna anayeweza kutabiri jambo lolote lile kwa uhakika.
Hivyo chochote unachohofia kuhusu kesho au siku zijazo, unajiumiza bure tu.

Unateseka zaidi kwa fikra zako kuliko kwa yale yanayotokea.
Unaumia kwa kudhani kuliko unavyoumizwa na matukio halisi.
Na hii yote inatokana na mtu kuacha kuishi kwenye wakati uliopo na kuanza kufikiria yale yajayo.

Kupunguza mateso haya ya kujitakia, ishi kwenye wakati uliopo. Fikra zako zote ziweke kwenye kile unachofanya kwa wakati husika.
Kila unapofikiria yajayo na kuhofia, jua mambo hayatatokea kama unavyodhani.
Jua kuna mengi mno yanayoweza kutokea ambayo huyajui, hivyo kuteseka nayo sasa siyo sahihi.

Na hata kama unachohofia kitatokea, kuhofia sasa haisaidii chochote.
Njia pekee ya kusaidia ni kufanya vyema kile unachofanya sasa, kuishi vizuri leo.
Muhimu kabisa, jiambie chochote kitakachotokea, utaweza kukabiliana nacho na kama huwezi basi utakubaliana nacho au kuachana nacho.

Huna haja ya kuteseka kwa mambo ambayo bado hujayafikia,
Maisha ni mafupi, yaishi leo kwa ukamilifu wake na kuyafurahia, ukifanikiwa kuiona kesho, iishi hivyo pia.
Lakini siyo kuipoteza leo kwa kuihofia kesho na kesho inapofika unaipoteza tena kwa kuhofia keshokutwa.
Kuishi hivyo ni kuchagua kuyapoteza maisha yako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu jukumu lako kuu, soma zaidi hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/12/25/2185

Rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani.