Asilimia zaidi ya 90 ya watu kwenye jamii hawaishi maisha yao.

Badala yake wanaishi maisha ya maigizo, maisha ya kufuata mkumbo.

Wengi wanaishi maisha ya kufanya kile kinachofanywa na wengine.

Kuishi hivyo ni rahisi, hakuna atakayekusumbua, kwa sababu unafikiri, kusema na kufanya kama wengine wanavyokubali.

Lakini ukichagua kuyaishi maisha yako, unalazimika kufikiri, kusema na kufanya tofauti na wengine.

Hilo linakuweka kwenye mgogoro mkubwa, kwani utakayofikiri, kusema na kufanya yatakuwa yanapingana kabisa na yale wanayokubali wengi.

Hivyo watakupinga, watakukosoa na hata kukutishia kwamba ukiendelea hivyo utatengwa kabisa.

Lazima uwe tayari kukabiliana na hayo kama kweli unataka kuyaishi maisha yako, lazima ujue umetangaza vita na wote wanaokuzunguka, ambao watatumia kila mbinu kuhakikisha watakuangusha.

Uzuri ni kwamba, utakapokuwa tayari kufikiri, kusema na kutenda kama unavyochagua wewe, utajisikia vizuri, utakuwa huru na hata kama watu hawatakuelewa sasa, kuna kipindi watakuja kukuelewa.

Hivyo kama kuna fikra tofauti zinakujia kupitia kujifunza na kutafakari, kama kuna kitu cha tofauti unataka kusema au kuna namna ya tofauti ya kufanya kile kinachofanyika, usisite kufanya hivyo. Jiandae kukabiliana na ugumu, lakini simamia kile kilicho sahihi.

Wote walioibadili dunia na tunaowakumbuka leo ni kwa sababu walikuwa tayari kusimamia walichoamini hata pale walipopingwa na kila mtu.

Kuiga ni rahisi, lakini vitu rahisi havijawahi kuleta mafanikio makubwa. Kuwa tofauti ni kugumu na kuna gharama, lakini matokeo yake huwa ni mazuri. Maisha ni yako na uchaguzi ni wako, chagua kilicho sahihi kwako sasa na kiishi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha