Kuna aina mbili za ushauri, unazopaswa kuzijua na jinsi unavyoweza kutumia kwenye kile unachopitia.

Aina ya kwanza ni ushauri wa wazi, huu ni ule ushauri unaotolewa kwa wazi na unaoweza kumlenga kila mtu. Mfano unaposoma makala yenye ushauri kuhusu biashara, kazi au fedha, inaweza kuwa na mambo mazuri, lakini mengi ni ya wazi, hayakugusi moja kwa moja.

Ushauri wa wazi huwa ni mzuri kwa sababu unakupa mwanga wa jinsi ya kutatua kile ambacho unapitia. Lakini n hatari kuchukua ushauri wa wazi na kuufanyia kazi kama ulivyo bila ya kuangalia kile hasa ambacho unapitia.

Aina ya pili ni ushauri wa moja kwa moja, huu ni ule ushauri ambao unamlenga mtu moja kwa moja na unaoendana na kile ambacho anakipitia. Hapa anayehitaji ushauri anakuwa ameeleza kile anachopitia na jitihada ambazo ameshafanya, kisha anayetoa ushauri anatafakari kwa kina na kumshauri namna bora zaidi ya kufanya.

Ushauri wa moja kwa moja unamgusa mtu mmoja na kile anachopitia, hivyo unakuwa na manufaa kwa sababu unaonesha hatua ambazo mtu anapaswa kuchukua kulingana na hali yake na alipo kwa sasa. Ushauri huu wa moja kwa moja siyo rahisi kutoa wala kupokea, unahitaji muda, kuelewa hali kwa kina na kisha kutafakari na kuona kipi mtu anapaswa kufanya.

Unapopokea ushauri, jua kama ni wa wazi au wa moja kwa moja.

Kwenye jamii, watu wengi ni watoaji wa ushauri, lakini huwa ni wa moja kwa moja na hupenda kulazimisha watu wafuate ushauri huo.

Mfano mtu anaona kwa mahusiano yako labda na ndugu zako, anakuambia huwasaidii ndugu zako kabisa, huwajali. Kumbe kwa ndani hajui ni mara ngapi umewasaidia na wakaishia kukuangusha. Kama mtu huyo angesikia hatua ambazo umeshachukua mpaka sasa na matokeo yaliyopatikana, angeona ni jinsi gani isivyo rahisi kutoa ushauri wenye manufaa.

Ushauri mwingi ambao watu wanakupa kabla hujawaomba huwa siyo ushauri wenye manufaa makubwa kwako, hivyo uchuje sana na angalia kwanza hali unayopitia na hatua ambazo umeshachukua kabla ya kufanyia kazi ushauri huo.

Na kama umekwama mahali na unataka ushauri, angalia ni nani sahihi kukushauri kwenye eneo hilo kulingana na uzoefu, kisha muombe mtu huyo akupe muda wake. Mweleze kwa ukweli na kina kile unachopitia, yote ambayo umeshafanya, matokeo uliyopata na ulipokwama. Baada ya kumweleza hayo na kukuelewa ndipo sasa akushauri namna bora zaidi ya kufanya.

Epuka sana watu unaowaeleza kitu kwa sekunde 30 na kukupa ushauri kwa dakika moja, ingekuwa rahisi hivyo, ungekuwa umeshatatua mwenyewe na isingekuwa changamoto kubwa kwako.

Na kwa upande wa pili, usiwe mwepesi wa kutoa ushauri kwa yale unayoyaona kwa nje, hasa pale ambapo mtu hajakuomba umshauri. Unaweza kutoa mapendekezo kulingana na kile unachokiona, lakini kwa ushauri, ni vyema mtu akakueleza kile anachopitia ndiyo uweze kumshauri, kama iko ndani ya uwezo wako.

Ushauri ni kitu ambacho watu hutoa na kupokea hivyo na kuishia kutokuwa wa manufaa kwao au kwa wengine. Kuwa makini sana na hilo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha