Wasiwasi huwa ni zao la msongamano wa mawazo na fikra kwenye akili yako. Akili inakosa nafasi ya kutosha kwa yale yaliyo muhimu.
Ni kama ilivyo kwenye chumba au ofisi ambayo haijapangiliwa vizuri, ukitaka kutafuta kitu, inakuchukua muda mrefu mpaka ukipate. Muda mwingi unaishia kwenye kupangua vitu visivyo na matumizi na vilivyo eneo lisilo sahihi.
Hivyo ndivyo akili zetu, usipozifanyia usafi na kuzipangilia, mawazo mengi yanasongamana, ambayo huna matumizi nayo. Hayo yanachukua nafasi kubwa na unapokuwa na mawazo ambayo una matumizi nayo hayapati nafasi.
Hivyo hatua ya kwanza kabisa kuchukua ili kuondokana na wasiwasi, hofu na mkwamo wowote unaokuwa unapitia ni kusafisha akili yako. Kuondoa kila aina ya uchafu na msongamano kwenye akili, ili kuwe na nafasi ya kutosha kwa yale muhimu yanayohitaji umakini wako.
Kuna njia mbalimbali za kufanya hivyo, hapa tutazigusia tatu muhimu za kuanza nazo.
Njia ya kwanza ni ya kuondoa kabisa takataka kwenye akili, hizi ni zile fikra zinazosongamana kwenye akili yako lakini hazina matumizi. Unaweza kufanya hivi kwa tahajudi (meditation) ambalo ni zoezi la kuituliza akili na kuondoa fikra zisizo na matumizi. Kwa kufanya tahajudi, unaifanya akili ipunguze msongamano wa fikra.
Njia ya pili ni kupunguza vitu kwenye akili ili kupata nafasi zaidi, vitu hivyo vinakuwa na matumizi, lakini siyo kwa sasa. Hivyo badala ya kuviacha vilete msongamano, unavipunguza na kuviweka eneo jingine. Unafanya hivyo kwa kuyapakua mawazo yako muhimu kutoka kwenye akili yako na kuyaweka kwenye maandishi. Kuna mawazo mengi mazuri unakuwa nayo na kujiambia utayakumbuka, hivyo unajilazimisha kuendelea kuyakumbuka wakati huna matumizi nayo sasa. Hayo unapaswa kuyapakua kwa kuyaandika mahali. Ukishayaandika huna haja ya kuendelea kujikumbusha, wakati unapoyahitaji unajua wapi utayapata. Kuwa na njia ya kuandika mawazo yako mazuri, inaweza kuwa kijitabu cha kuandika (notebook) au programu ya simu/kompyuta ya kuhifadhi mawazo yako.
Njia ya tatu ni kupangilia vizuri vile vinavyobaki kwenye akili yako na vyenye matumizi. Kuna mawazo na fikra ulizonazo na ambazo unazitumia, lakini unaziacha zinazagaa hovyo kiasi cha kuleta fujo kwenye akili. Hizi unapaswa kuzipangilia vizuri. Unafanya hilo kwa kugawa majukumu yako kwenye makundi na kisha kutenga muda wa kundi husika. Mfano kama unataka kuwasiliana na watu mbalimbali, tenga muda wa kufanya mawasiliano na katika muda huo wasiliana tu. Kama unafanya kazi, kusanya yale mawazo na fikra zote kuhusu kazi husika na fanya kazi hiyo tu. Unapojivuruga ni pale unapofanya kazi, huku unafikiria kuwasiliana na watu na mengine, hapo unaivuruga akili na kuishia kuwa na wasiwasi na hofu.
Kusafisha akili ni zoezi endelevu, zoezi la kufanya kila siku na mara nyingi kwa siku. Akili ni rahisi kuchafuka kwa sababu kuna watu na vitu vingi vinapambana kupata umakini wetu, tusipokuwa wakali kuulinda na mara kwa mara kuisafisha, tutajikuta kila siku tumejawa na wasiwasi na hofu, huku siku zikianza na kuisha na hakuna kikubwa tunachokuwa tumekamilisha.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,