Habari rafiki yangu mpendwa,

Kama ambavyo nimekuwa nakushirikisha kwenye makala na vitabu mbalimbali, nimekuwa siyo mfuatiliaji wa habari kwa muda mrefu na mwaka 2018 nilijiondoa kwenye mitandao yote ya kijamii.

Lakini yale mambo makubwa na mbalimbali yanayoendelea duniani, hayajawahi kunipita. Hivyo watu wengi wamekuwa wananiuliza ninawezaje kujua yanayoendelea licha ya kutokuwa mfuatiliaji wa habari?

Kwenye makala hii nakwenda kukushirikisha njia ambazo nimekuwa natumia kupata maarifa ambayo yana manufaa kwangu na siyo taarifa za kunichosha lakini hazina manufaa.

Siku za karibuni kumekuwa na matukio makubwa yanaendelea duniani, na mawili ambayo niliyashirikisha na watu wakauliza nimepataje taarifa hizo ni Elon Musk kuwa tajiri namba moja duniani na Donald Trump kufungiwa na mitandao mikubwa ya kijamii.

Kabla sijaeleza kwa nini nimejua yaliyotokea kwa watu hao wawili, historia fupi kidogo inahusika, kwa wale ambao hawajanijua kwa muda mrefu. Tuanze na hiyo picha hapo chini;

Picha niliyotengeneza 2015 kushoto mimi na kulia ma role model wangu watatu

Mwaka 2015 nilishirikisha picha yangu ikiwa na picha nyingine tatu na kueleza watu hao wengine watatu ndiyo ma ROLE MODEL wangu, watu ambao ninajifunza kwa kina kutoka kwao kulingana na yale waliyofikia kwenye maisha yao.

Wa kwanza kwenye picha ni Elon Musk, nilimchagua awe Role Model wangu kwa sababu ni bilionea na moja ya malengo yangu makubwa ni kuwa bilionea. Lakini licha tu ya kuwa bilionea ni mtu aliyeanzia chini, aliyepambana sana na mara zote amekuwa akienda kinyume na kundi.

Wa pili kwenye picha ni Winston Churchill, huyu alikuwa waziri mkuu wa Uingereza ambaye alipambana na kuivusha dunia katika kipindi kigumu, wakati wa vita ya pili ya dunia. Huyu naye alipitia magumu mengi, ikiwepo kuwa nje ya siasa kwa miaka kumi, kipindi ambacho alisoma na kuandika vitabu vingi, kitu kilichompa uelewa mkubwa. Huyu nina mengi ya kujifunza kwake kuhusu uongozi na uandishi pia.

Wa tatu kwenye picha ni Seneca, ambaye alikuwa mwanafalsafa wa Roma ya kale wa shule ya falsafa iitwayo Ustoa (Stoicism). Nimemchagua Seneca kwa sababu tatu, moja ni falsafa ya Ustoa, hii ni falsafa bora kabisa kuendesha maisha. Mbili ni uandishi, Seneca aliandika maandiko mengi mno, mengi yalipotea na machache yaliyosalia ni hazina kubwa na moja wapo ni barua 124 alizoandika kwa rafiki yake Lucilius, amegusa kila kona ya maisha. Na tatu ni ushiriki wake kwenye siasa, kwanza aliwekwa uhamishoni kwa kipindi kirefu, pili alimlea mtawala wa Roma aliyeitwa Nero na tatu alihukumiwa kifo na kujiua na mtawala aliyemlea mwenyewe. Seneca ni mtu ambaye nimekuwa najipima kwake kwa kila ninachofanya.

Baadaye niliongeza watu wengine kwenye orodha hiyo Donald Trump kwenye ubilionea na uongozi, Seth Godin kwenye uandishi na mafunzo, Grant Cardone kwenye fedha na uwekezaji, Gary Vee kwenye kuweka juhudi ya kazi na Dan Pena kwenye ukocha.

Hivyo kama unavyoona orodha hiyo, kwa wale ambao hawapo hai nimekuwa nasoma vitabu vyao na vilivyoandikwa kuhusu wao. Na kwa wale walio hai nimekuwa nafuatilia kila wanachofanya, iwe ni kizuri au kibaya ili kujifunza. Na hilo ndiyo lililopelekea nipate taarifa za wawili hao mapema kabisa, kwa sababu nafuatilia mengi kuwahusu.

Kwa muda sasa nimekuwa nashauri watu waachane kabisa na habari, usiangalie habari za tv, usisikilize habari za redio na usisome magazeti. Na hoja yangu kuu ni kwamba habari nyingi ni hasi, hazina manufaa kwako na zinachukua muda na umakini wako ambao ungeutumia kwa vitu vingine kama kusoma vitabu, ungenufaika zaidi.

Na sasa nimekuwa nashauri sana watu kuachana kabisa na mitandao ya kijamii, hasa kwa matumizi binafsi kwa hoja kwamba mitandao hii inavuruga utulivu wako na kukugeuza kuwa mtumwa unayefanyishwa kazi na kuwatajirisha wengine.

Kama unavyojua, hakuna kitu kinachokubalika na wote, wapo ambao wamekuwa wananipinga kabisa kwenye hayo na kuona ni kujinyima mambo mazuri, hao huwa hata sibishani nao, kama vitu hivyo vina manufaa kwao, wanapaswa kuendelea, mimi ni nani mpaka niwapangie maisha?

Ninaowalenga zaidi ni wale ambao wamechoshwa kweli na vitu hivyo, yaani habari na mitandao ya kijamii, wanatamani sana wangeachana navyo, lakini wanahofia kwamba wasipofuatilia basi watapitwa na yale yanayoendelea.

Hawa nawaelewa, kwa sababu ni hitaji letu sisi binadamu kujua kila kinachoendelea, hasa kwenye maeneo yanayotuhusu. Lakini kutegemea habari au mitandao ya kijamii kujua yale yanayoendelea ni sawa na kuzama kwenye shimo lisilo na ukomo, unazama na kuzama na hakuna mwisho.

Leo nimeandaa makala hii kuondoa hofu hiyo, kwa wale ambao wanatamani sana kuachana na habari na mitandao ya kijamii na hawataki wabaki gizani.

Hapa nakwenda kukushirikisha njia saba za kujua yale muhimu yanayoendelea kama unachotaka ni mafanikio makubwa kwenye maisha yako na siyo kusumbuka na mambo ya udaku na yasiyo na manufaa.

Moja; kuwafuatilia waandishi moja kwa moja.

Waandishi wengi ambao nimekuwa nasoma na kufuatilia kazi zao, nimejiandikisha kwenye mifumo yao ya kutuma email na hivyo huwa napokea taarifa mbalimbali kutoka kwao moja kwa moja.

Kupitia njia hiyo najua vitabu wanavyotoa, vitabu wanavyopendekeza kusoma na mengine muhimu yanayoendelea kwenye eneo wanaloandikia.

Nimejiandikisha kwa waandishi wengi lakini wachache ambao wanatuma email karibu kila siku na najifunza sana kwao ni  Seth Godin, Ryan Holiday, Robin Sharma, Tim Ferris, Carl Newport, Ramit Seth, James Altucher, Mark Manson, Gretchen Rubin, James Clear, Morgan Housel na wengine.

Unaweza kuchagua orodha ya waandishi kulingana na eneo unalopenda kufuatilia au kujua zaidi, kisha kuwafuata moja kwa moja kwa kujiunga kwenye email newslater zao.

Mbili; mtandao wa Substack.

Kuna mtandao mpya ambao unawakusanya waandishi kwa pamoja na wanautumia kuandika makala ndefu na zenye mambo ya kina kuliko zile zinazoandikwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari.

Kupitia mtandao huo unaweza kuchagua eneo gani unataka kujifunza zaidi na hapo utawapata waandishi waliobobea kwenye eneo hilo, ambao wanaandika makala zinazokupa mafunzo ya kina na yenye manufaa.

Tatizo la makala nyingi za mitandaoni, hasa kwenye mitandao ya kijamii huwa zimeandikwa kunasa umakini wako (click bait) kwa lengo la kuuza matangazo, hivyo hazitoi mafunzo ya kina.

Kwenye substack hakuna hilo, mwandishi anaandika kwa kina na siyo kuteka hisia.

Ingia www.substack.com na uchague ni eneo gani unapenda kujifunza zaidi na utawaona waandishi wazuri kwenye eneo husika. Baadhi ya makala kwenye mtandao huo ni za kulipia na kuwa mwanachama ili usome, lakini zipo nyingi za bure ambazo ni nzuri mno.

Tatu; mtandao wa Twitter.

Unaweza kushangaa hapa, nimekuambia uondoke kwenye mitandao yote ya kijamii, lakini tena nakuambia utumie twitter kujua yanayoendelea, je hapo si unarudi kule kule?

Jibu ni hapana, nakwenda kukupa siri ya kutumia twitter bila ya kusumbuliwa nayo. Siri hiyo ni kwenda moja kwa moja kwenye profile ya mtu unayemfuatilia. Uzuri wa twitter ni kwamba unaweza kuingia kwenye profile bila ya kuwa na akaunti kabisa, ni kujua tu anwani yake na kuingia.

Kwa mfano mimi kuna watu wanne ambao huwa naingia kwenye profile zao moja kwa moja kwenye twitter, ambao ni Elon Musk (www.twitter.com/elonmusk), Naval Ravikant (www.twitter.com/naval), Nassim Taleb (www.twitter.com/nntaleb) na Kapil Gupta (www.twitter.com/KapilGuptaMD).

Elon namfuatilia kwa sababu nimechagua kujifunza kutoka kwake, Naval kwa sababu napenda falsafa yake ya utajiri na furaha, Taleb napenda utata wake na Kapil nimemjua kupitia Naval, naye ana falsafa ngumu kidogo inayotikisa mengi ninayoamini.

Uzuri wa kwenda kwenye profile ni unasoma yale ambayo mtu unayemfuatilia ameshirikisha na huhangaiki na mengine hata maoni ambayo watu wanakuwa wameweka.

Unaweza kuchagua watu unaopenda kuwafuatilia na kujifunza kwao, jua anwani zao za twitter kama wanatumia mtandao huo na kuwa unaingia kwenye profile zao kwa kadiri unavyojipangia mwenyewe.

Nne; majarida makubwa.

Kuna majarida makubwa ambayo huwa yanaandika kwa kina mambo yanayoendelea kwenye tasnia husika. Hayo huwa ni mazuri kwa sababu yanakuwa na makala na tafiti zinazokupa maarifa sahihi kwenye eneo hilo badala ya usumbufu wa kwenye vyombo vingine vya habari na mitandao ya kijamii.

Kila tasnia ina majarida yake, kwa upande wangu kwa yale ninayofuatilia, kuna majarida matano ambayo nimejiandikisha na huwa napokea barua pepe kunapokuwa na vitu vipya. Majarida hayo ni;

1. Forbes, ambapo najifunza mengi kuhusu mabilionea na mafanikio kwa ujumla, anwani yake; www.forbes.com

2. Entrepreneur, ambapo najifunza mengi kuhusu ujasiriamali kwa ngazi ya dunia, anwani yake; www.entrepreneur.com

3. Tanzania Invest, ambapo najifunza yale yanayoendelea kwenye biashara na uwekezaji Tanzania, anwani yake; www.tanzaniainvest.com

4. Business Daily Africa ambapo najifunza yale yanayoendelea kwenye biashara na uwekezaji Afrika, japo mengi ni ya Kenya, anwani yake; www.businessdailyafrica.com

5. The New England Journal Of Medicine ambapo najifunza yanayoendelea kwenye sekta ya afya, anwani yake; www.nejm.org

Kwa tasnia uliyopo au yale unayotaka kujifunza na kubobea, chagua majarida yanayohusika kisha yafuatilie, jiandikishe kwa barua pepe na watakuwa wanakutumia moja kwa moja.

Tano; 3 Quarks Daily

Unataka kuzisoma makala bora kabisa zilizopo kwenye mtandao wa intaneti bila kuhangaika sana? Kama jibu ni ndiyo basi kuna mtandao unaoitwa 3 Quarks Daily (https://3quarksdaily.com) ambao unakusanya makala bora kabisa zilizopo mtandaoni kwenye maeneo ya sayansi, sanaa, falsafa na siasa na kuzileta pamoja.

Kwa kufuatilia mtandao huo, huna haja ya kuhangaika kutafuta huku na kule, wewe yote unayakuta pamoja.

Ipo mitandao mingi ambayo inakusanya makala hivyo, lakini mtandao huu unakusanya zile zilizoandikwa kwa kina na zenye maarifa yenye manufaa.

Tembelea mtandao huo mara kwa mara na peruzi, utakutana na mambo mazuri unayoweza kunufaika nayo.

Sita; Jamii Forums

Kama unataka kujua yale yanayoendelea kwa Tanzania, basi sehemu inayokusanya yote ni mtandao wa Jamii Forums.

Zamani mtandao huu walikuwa na njia ya kuonesha makala zinazosomwa sana na ikikuwa rahisi kupata picha ya yale yanayoendelea. Lakini siku hizi wameondoa njia hiyo, hivyo njia rahisi ya kujua makala zinazosomwa au kujadiliana sana ni kwenda kwenye eneo la makala mpya (www.jamiiforums.com/whats-new)

Mtandao huu una vitu vingi sana na kwenye majadiliano kuna mengi, hivyo unapaswa kuwa makini sana. Ni eneo la kuchungulia tu kujua yapi yanayoendelea, lakini epuka kuzama kusoma kila kitu, inavutia kufanya hivyo lakini utachoka na kuondoka bila manufaa.

Uzuri wa mtandao huo kuna majukwaa ya biashara, kilimo, elimu, afya na kadhalika, hivyo unaweza kuingia moja kwa moja kwenye jukwaa husika na kujua yapi yanaendelea.

Unahitaji kuchambua vizuri maana kuna mengi mazuri na mengi zaidi ambayo siyo mazuri.

Saba; mitandao mingine.

Kuna mitandao ambayo zamani nilikuwa naitumia lakini siku hizi siitumii, nayo pia ina mambo mazuri lakini kwa miaka ya karibuni imeshambuliwa na watu wasio makini na kugeuka kuwa usumbufu. Mitandao hiyo ni Quora (https://www.quora.com), Medium (https://medium.com) na Reddit (https://www.reddit.com).

Na pia kuna mitandao ambayo huwa naitembelea mara moja moja, hasa ninapokuwa nataka kupata kitu cha kunichekesha, mitandao hiyo ni Dilbert (https://dilbert.com) ambao ni wa katuni na The Babylon Bee (https://babylonbee.com) ambao unaandika habari feki zinazofanana na ukweli, ila za kuchekesha.

Unapata wapi muda wa kusoma yote hayo?

Rafiki, kwa kuangalia hayo niliyoorodhesha hapo kwa siku huwa napokea barua pepe zisizopungua 30. Hivyo unaweza kujiuliza napataje muda wa kusoma zote hizo?

Jibu ni sisomi kila kitu, huwa natenga muda wa kupitia zote kwa haraka na kuchagua zile nitakazozisoma kwa kina. Kwa njia hiyo napata picha kubwa ya yale yanayoendelea na kisha kuchagua yale ninayotaka kujua kwa undani zaidi.

muonekano wa email kwenye eneo la updates ambapo napokea taarifa kutoka kwa waandishi niliojiandikisha kwao.

Nimeshirikisha hili kwa sababu linaweza kuwa msaada kwa wengi ambao wanapenda kuwa na uelewa mpana wa mambo muhimu yanayoendelea kwenye sekta na tasnia zinazowahusu. Siyo lazima usome yale ninayosoma mimi, bali yatumie kujifunza kutengeneza mfumo utakaokuwezesha kujifunza yale muhimu na kuondokana na usumbufu wa habari na mitandao ya kijamii, ambayo inakazana kunasa umakini wako ili inufaike kifedha.

Chagua sasa kutawala umakini wako badala ya kugeuzwa kuwa mtumwa na mitandao isiyokupa chochote chenye manufaa zaidi ya kuchochea hisia zako. Mtandao wa intaneti ni mpana, huwezi kumaliza wote, lakini kwa kuchagua maeneo yako machache unayotaka kuwa na uelewa mpana na kisha kuwafuata wachache wanaoyajadili kwa kina, itakuwa na manufaa kwako.

Karibu uendelee kujifunza kupitia AMKA MTANZANIA (www.amkamtanzania.com) sehemu pekee unayopata makala bora za maendeleo binafsi na mafanikio bila ya usumbufu wa matangazo au kelele nyingine zilizopo mtandaoni.

Rafiki, karibu upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania