Kila mzazi anaweza kumwamasisha mtoto wake na kisha akafanya makubwa. Kwa sababu kila mzazi ni mwalimu wa kwanza kwa mtoto wake.

Watoto wanahamasika kutoka kwa wazazi wao. Pale wanapoona wazazi wanajituma na kufanya makubwa. Kwa mfano, watoto wakiona wazazi wanafanya mazoezi pamoja nao wanahamasika kufanya bila shuruti. Lakini wazazi wakiwa wanawaambia watoto wafanye mazoezi halafu wao hawafanyi watoto wanakuwa hawahamasiki.

Je ni namna gani mzazi unaweza kumwamasisha mtoto wako na kufanya makubwa?

Mzazi yeyote anaweza kumwamasisha mtoto wake kwa kufanya neno lako kuwa sheria. Yaani kila unachomwahidi mtoto wako kitekeleze.

Kila mpango wako uliojiwekea jitahidi kuufanyia kazi. Mtoto anapomuona mzazi anawajibika kwa mipango yake naye anakuwa ana hamasika naye kufanya makubwa.
Katika mipango yako mikubwa uliyoweka unaweza ukamshirikisha hata mtoto wako halafu muoneshe na hatua unazochukua zitamwamasisha kuchukua hatua.

Ukimshirikisha mtoto wako malengo yako makubwa na akiona unayafanyia kazi naye anahamasika kujituma kuwa kama wewe. Kwa mfano, Kama mtoto anajua wewe huwa unaamka mapema naye atajituma kuhakikisha anakuwa kama wewe kwa kuamka mapema.

Ukiwa mzazi unasoma vitabu, halafu unachukua hatua kwa kile unachojifunza na mtoto anakuwa anahamasika kweli.

Kuwa mtu wa mfano kwa mtoto wako mwenyewe. Aone kweli mambo yanawezekana na hivyo naye atajituma sana. Wazazi wakiamka na watoto wanaamka.

Mtoto wako anakua vile ambavyo wewe unakua. Ni bora uanze kumwambukiza tabia chanya mapema kabla hajaanza kutengeneza tabia zake kutoka kwa watu wengine.

Tunatengeneza tabia kisha tabia zinatutengeneza. Hivyo ukitengeneza tabia kwa mtoto wako tabia zitakwenda kumtengeneza na kuwa vile unavyotaka.

Kila kilicho bora huwa kinaandaliwa na kulipiwa gharama. Hivyo kwa kuwa malezi ni kazi nakusihi weka kazi.

Kama mzazi unavyojituma na kuweka nguvu katika kukusanya fedha vivyo hivyo unapaswa kuweka kazi katika malezi. Msaidie mtoto wako kwa kumjengea misingi mizuri ambayo itakuja kumsaidia baadaye.

Hatua ya kuchukua leo; Kaa na mtoto wako, mshirikishe baadhi ya malengo yako ambayo anaweza kuona hatua unazochukua na yeye akawa anapima matokeo. Kwa mfano, Kama ni lengo lako ni kuboresha afya muoneshe mpango wako wa kwenda kutekeleza maazimio yako.

Neno lako liwe sheria. Kile unachoahidi kitekeleze. Usioneshe sababu kwa mtoto naye atajifunza kuwa mtu wa sababu.

Kuwa mtu wa matendo chanya, chukua hatua kubwa mpaka zile hatua unazochukua zimbariki mtoto wako naye ahamasike.

Mtoto wako hawezi kuwa tofauti kama na wewe unaishi kimazoea. Unafanya yale yale kwa mtindo ule ule huku ukitegemea kupata matokeo tofauti. Kupata matokeo tofauti, chukua hatua tofauti.

Makala hii imeandikwa na
Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali.

Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa
http://kessydeo.home.blog vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI. Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,
Mwl, Deogratius kessy
0717101505/0767101504
deokessy.dk@gmail.com //
Asante sana