Kwa asili binadamu huwa tunapenda kushindana, mweleze mtu matatizo yako naye atakuambia hayo yako si kitu, atakueleza matatizo yake ambayo ni makubwa zaidi.

Unaweza kuwa unaendesha gari barabarani na mbele yako kuna mtu mwingine anaendesha taratibu tu, anaonekana kutokuwa na haraka. Unaamua umpite kwa sababu una haraka na kile kitendo tu cha kuomba kumpita, anaanza kukaza mwendo. Na hata ukimpita anaanza kukukimbiza ili akupite tena.

Hivyo ndivyo tulivyo, ndani yetu tunapenda sana mashindano. Na hilo ndiyo limekuwa linaleta hali ya watu kutokuelewana, hasa kwenye mahusiano mbalimbali, kwa sababu ya mashindano.

Sasa kwenye zama hizi, mashindano ni kama yamechochewa zaidi, kama ni moto basi umemwagiwa petroli na kilichofanya hivyo ni mitandao ya kijamii.

Kabla ya mitandao ya kijamii, ulikuwa unasukumwa kushindana na wale wanaokuzunguka, kwenye kazi, biashara au jamii. Unaona mwenzako kafanya kitu fulani na wewe unasukumwa kufanya pia.

Lakini baada ya kuja kwa mitandao ya kijamii, mashindano yamekuwa ni ya dunia nzima, siyo tu kwa wale wanaokuzunguka, bali kwa wengi unaowaona mtandaoni.

Umeona mwenzako kaweka picha anafanya starehe, na wewe unasukumwa kufanya hivyo pia. Unaona wengine wana wafuasi wengi na wewe unakazana uwe na wafuasi pia. Kila unachoona kwa wengine kwenye mitandao, unapata msukumo wa wewe kufanya pia.

Na hapo ndipo unapaswa kuwa makini, kujichunga na kujihoji. Kabla hujakimbilia kuchukua hatua jiulize mashindano unayoingia yanakufikisha wapi.

Ipo kauli kwamba tatizo la mbio za panya ni hata ukishinda unabaki kuwa panya. Hivyo mashindano mengi unayoshiriki, ni yasiyo na manufaa, kwa sababu hata ukishinda, haikubadilishi chochote.

Sawa, mtu ameeleza matatizo yake na wewe ukaeleza yako ambayo ni makubwa zaidi, umepata nini? Umeona wengine mitandaoni wanafanya vitu fulani na wewe ukafanya, mwisho umenufaikaje?

Muda wako ni mfupi, nguvu zako zina ukomo, unapotumia rasilimali hizo kwa mambo yasiyo muhimu, unajipunja kuzitumia kwa mambo yenye tija kwako. Angalia matokeo ya kila kitu kabla hujawekeza rasilimali hizo ili usizipoteze.

Na mara nyingi sana, jizue kushindana. Pale unapoona watu wanafanya kitu au wanaeleza kitu, kuna msukumo ndani yako unakutaka ufanye au kueleza ili uonekane wewe ni zaidi. Uzuie sana msukumo huo kama hakuna chenye manufaa utakachopata kwa kufanya hivyo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha