Tukisikia mambo ya kura, fikra zetu zinakwenda moja kwa moja kwenye uchaguzi wa kisiasa au wa aina nyingine.

Tunajua kwenye chaguzi hizo, wagombea wanakuja kujinadi kwetu, wakitupa sera zao na kutuambia kwa nini tuwachague. Kisha tunaangalia na kuona mgombea yupi sahihi na kumpa kura yetu.

Kitu ambacho huelewi ni kwamba, kila siku unauziwa sera na unapiga kura, kila siku ya maisha yako. Kwanza nikisema kila siku sioneshi msisitizo, ni kila sekunde ya kila dakika ya kila saa kwenye siku yako.

Kwenye maisha yako una rasilimali nyingi ambazo zina uhaba, na hivyo huwezi kuzitumia bila ukomo na hapo ndipo dhana ya kupiga kura inapokuja.

Chukua mfano umepata pesa, iwe umepokea mshahara au umepata faida kwenye biashara, mbele yako unakuwa na mahitaji mengi ya kifedha kuliko kiasi ulichonacho. Hivyo hapo lazima upime mahitaji yapi muhimu zaidi na uyape pesa hiyo.

Huenda umewahi kujiuliza kwa nini ukiwa na pesa kuna wakati unafanya manunuzi ambayo baadaye unayajutia? Jibu ni hili, wale wanaokushawishi uwapigie kura kwa fedha zako wanakuwa wamekushinda. Chukua mfano umetoka nyumbani, huna mpango wa kununua nguo mpya, unakutana na muuza nguo na anakuambia ana nguo nzuri na siku hiyo kuna punguzo la asilimia 50, punguzo ambao halitakuja kutokea tena. Mara moja unabadili kura yako, ulikuwa na mipango mingine, lakini sasa unaona nguo hiyo ni kipaumbele zaidi.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye rasilimali nyingine muhimu ambayo kila mtu analalamika hana, ambayo ni muda. Muda ni changamoto, kila mtu hana muda. Lakini ukweli ni kwamba muda haujawahi kupungua, ni ule ule, ila mambo ya kufanya ndiyo yamekuwa mengi. Hivyo kinachotokea ni ushawishi unaokuja kwako kwa kipi ukipe kura yako.

Una kitabu cha kusoma mbele yako, una simu janja yenye mitandao ya kijamii mbele yako na una habari mbele yako, kura yako unaipeleka wapi? Ukishachagua kufanya kimoja, maana yake umeamua kuacha kufanya kingine. Kadhalika kwenye kazi, mahusiano na mengine. Kuna vitu vingi vinagombea muda wako, kura yako unaipeleka wapi ndiyo kinachoamua una muda au huna.

Kama unajiambia huna muda wa kufanya kitu fulani siyo kwa sababu umeianza siku hiyo ukiwa na mapungufu, bali umepiga kura yako kwa kuchagua kufanya vitu vingine. Kama huna muda wa kusoma vitabu ni kwa sababu umechagua kufanya vitu vingine na muda huo.

Swali ni je yale unayochagua kufanya na muda wako yana manufaa kwako? Je ni bora kuliko yale unayoshindwa kufanya kwa sababu huna muda? Utauziwa sera nyingi, lakini wewe ndiye mpiga kura, kura yako unaipigia upande upi? Hayo ni maamuzi yako.

Umakini na nguvu za mwili wako ni maeneo mengine ambayo unapiga kura kila wakati kwenye maisha yako. Ukishaamua kupeleka umakini au nguvu zako kwenye kitu kimoja, maana yake umeachana na vingine. Swali linarudi kwenye kipaumbele, kipi muhimu zaidi?

Tambua maisha yako yote ni kupiga kura, tambua kila kinachokuja mbele yako kinapiga kampeni. Kama ilivyo kwenye kampeni za kisiasa, tunajua kabisa wengi wanadanganya, hivyo pia ndivyo yale yanayoshawishi uyapigie kura kila siku, yanakudanganya na kukuhadaa, ukishayapa kura umepoteza.

Mfano wa vitu vinavyodanganya kwenye kura unazopiga kila siku ni mambo rahisi kufanya kama kuperuzi mitandao, kufuatilia habari na mengine yasiyo muhimu. Yatakushawishi ni muhimu, utajua yanayoendelea na utajisikia vizuri. Lakini ukishakubali, unajikuta umepoteza muda, umakini na nguvu zako kuhangaika na mambo yasiyo na manufaa yoyote kwako.

Kila sekunde ya maisha yako jua unapiga kua, kuwa makini na kura zako, chagua yale yenye manufaa kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha