Karibu rafiki yangu mpendwa kwenye makala hii ya ushauri wa changamoto zinazotuzuia kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yetu.

Kama tunavyojua, changamoto huwa hazikosekani kwenye maisha, na kuzitatua ndiyo njia pekee ya kupiga hatua na kufanikiwa kwenye maisha yetu.

Hapa tunakwenda kujifunza jinsi ya kufanya maamuzi iwapo ujiendeleze kielimu au ufanye biashara.

Hii ni hali ambayo imekuwa inawaweka wengi njia panda na kushindwa kujua ni wafanye lipi katika hayo mawili. Tunakwenda kujifunza jinsi ya kufikia maamuzi sahihi kwenye hili.

Tupate kwanza maoni ya msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili;

“Mimi ni mtumishi wa umma, ninawaza kwenda kujiendeleza kielimu au nitumie hiyo hela ya ada kufungua biashara ya stationary?” – Valency M.

Kama alivyotuandikia msomaji mwenzetu Valency, ni wengi wanaokuwa wamekwama kwenye changamoto ya aina hiyo.

Kwa kawaida, kwenye njia panda ya aina hii, huwa jibu lako ni la moja kwa moja, fanya vyote kwa pamoja.

Lakini kwa jinsi alivyotuandikia Valency, na kwa walio wengi, kuna uhaba wa rasilimali muhimu ambayo ni fedha. Ndiyo maana ameuliza iwapo atumie fedha kwenye ada au aitumie kuanzisha biashara, kinachomkwamisha kufanya vyote ni uhaba wa fedha.

Lakini pia japo hajasema, muda utakuwa kikwazo kingine, masomo yanahitaji muda na biashara pia inahitaji muda. Masomo huenda yatampeleka mbali na anapopanga kuanzia biashara, hivyo atashindwa kuisimamia kwa karibu na hivyo kuwa changamoto zaidi.

Hivyo anabaki njia panda, ajiendeleze kimasomo na asifungue biashara au afungue biashara na asijiendeleze kimasomo.

Ushauri wa kipi cha kufanya hapa unaanza na mtu mwenyewe, kwa kujitambua na kujua nini anataka kwenye maisha, pamoja na ndoto kubwa alizonazo.

Njia zote mbili ni sahihi, kujiendeleza kimasomo ni sahihi na kuanzisha biashara ni sahihi, ila usahihi huo unategemea malengo na ndoto kubwa alizonazo mtu.

Kwa mfano kama lengo lako ni kupanda cheo kwenye ajira na kufika ngazi za juu ambapo utalipwa vizuri, kujiendeleza kimasomo ni hatua sahihi, kwani hiyo inakufikisha kwenye lengo.

Na kama lengo lako ni kuwa huru, kuondoka kwenye ajira hiyo na kujiajiri mwenyewe, kuanza biashara ni hatua sahihi, kwani itakuwa mwanzo wa kutengeneza uhuru wako nje ya ajira.

Najua waelimishaji na wahamasishaji wengi hapa wangekuambia achana na kujiendeleza kielimu kwani unajiweka kwenye utumwa zaidi, fanya biashara. Lakini kuna watu wana ndoto ambazo njia pekee ya kuzifikia ni kupitia mfumo wa elimu. Mfano mwalimu ambaye anataka kuwa profesa wa chuo kikuu, hapo lazima upitie njia ya elimu. Au mtumishi ambaye anataka kufika ngazi za juu, lazima upate elimu.

Muhimu ni ufanye ukiwa unajua wazi kwamba katika kutimiza ndoto yako, kuna uhuru unajinyima, lakini pia njia unayotumia bado haikuhakikishii kufikia ndoto hiyo. Lakini kama upo tayari kupambana, hakuna kinachoshindikana.

Lazima pia ujue kwamba njia zote hazitakuwa rahisi, kila njia ina vikwazo na changamoto zake. Haimaanishi kwamba kwa kuwa una mtaji basi ukifungua biashara ndiyo umeshakuwa huru. Utafungua biashara na kipindi cha mwanzo kitakuwa kigumu, huenda biashara isipate faida, huenda hata ikafa kabisa. Lakini yapo mengi ambayo utajifunza na kama utaendelea basi utaweza kufanikiwa sana.

Jitambue wewe mwenyewe, jua nini unataka kwenye maisha, jua ndoto kubwa ambayo unataka kuifikia kisha kuwa tayari kulipa gharama katika kuifikia.

Kama utachagua kujiendeleza kielimu kwa lengo la kupanda cheo na kuongeza kipato, jua unaweza kuvipata hivyo, lakini ukakosa uhuru. Hivyo kama uhuru kwako siyo jambo muhimu zaidi, nenda njia hiyo.

Na kama utachagua kuacha kujiendeleza kielimu na ukafanya biashara, jua mwanzo utakuwa mgumu, utakabiliana na mengi lakini kama hutakata tamaa, utajijengea uhuru mkubwa kwa baadaye. Na muhimu kabisa, ukishakuwa huru, utaweza kujiendeleza kielimu kwenye kile unachotaka kujua na siyo kwa lengo la kupanda cheo au kuongeza kipato zaidi.

Kufanya maamuzi haya lazima uwe tulivu, lazima ujitafakari ulipotoka, ulipo na unapokwenda. Na muhimu zaidi, kuwa tayari kulipa gharama kupata kile unachotaka.

Hakikisha unasoma vitabu vya ELIMU YA MSINGI YA FEDHA na ELIMU YA MSINGI YA BIASHARA ili viwe mwongozo kwako kwa chochote utakachochagua katika hayo mawili. Kupata kitabu wasiliana na 0752 977 170.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania

Rafiki, karibu upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp