Mshumaa unapowashwa kwenye chumba chenye giza, huwa unatoa nuru kwenye chumba kizima. Mshumaa huo hautaisha haraka iwapo utawekwa kwenye chumba kikubwa kuliko chumba kidogo.
Kadhalika mshumaa huo hautaisha haraka kwa kuwasha mshumaa mwingine.
Mawimbi ya bahari yanapoinuka, huwa yanainua kila kilicho kwenye bahari hiyo, hakuna kinachoachwa chini na wimbi linaloinuka.
Hii ni mifano miwili rahisi kabisa inayotuonesha jinsi ambavyo asili inafanya kazi yake, kwa kutoa manufaa kwa wote.
Na hivyo ndivyo maisha yetu yanavyopaswa kuwa pia, kuhakikisha tunaishi maisha yanayogusa maisha mengine.
Chochote tunachofanya, kiwe na manufaa kwa wengine, kwa sababu haitupunguzii chochote.
Ukienda kazini na ukaifanya kazi yako kwa mazoea au kwa kusubiri kusukumwa, bado utatumia masaa yale yale na nguvu zile zile. Kadhalika ukiifanya kazi hiyo kwa hamasa na upendo, muda na nguvu ni ile ile. Wakati kufanya kwa mazoea na chuki hakuna manufaa, kufanya kwa hamasa na upendo kuna manufaa makubwa kwako, kwa nini usifanye kwa hamasa na upendo?
Kadhalika kwenye biashara, unaweza kuona mteja ni msumbufu na usizingatie katika kumhudumia vizuri, lakini muda na nguvu ni zile zile kama ungemchukulia ni mwelewa na mwenye uhitaji.
Mabadiliko kidogo tu kwenye mtazamo wako kwa kile unachofanya, yanatosha kuleta mabadiliko makubwa kwenye matokeo, kwako binafsi na kwa wale wanaoguswa na kile unachofanya na hilo litakufikisha kwenye mafanikio makubwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Ni kweli kocha, ni busara kuishi maisha yanayogusa maisha mengine.
LikeLike
Kabisa.
LikeLike
Asante sana Kocha
LikeLike
Karibu
LikeLike