Kusoma kunafanana kabisa na kula, kama unavyoupa mwili virutubisho kupitia chakula, ndivyo unavyoipa akili virutubisho muhimu kupitia usomaji.
Unajua kwenye ulaji unakula chakula kingi, kinameng’enywa na kisha sehemu kidogo ya chakula hicho inafyonzwa mwilini na kutumika kwenye kuujenga mwili. Sehemu kubwa inayobakia unaitoa kama uchafu kupitia kinyesi.
Kwenye usomaji, unaweza kusoma vitu vingi, lakini vichache ndiyo vitakuingia, utavielewa vizuri na kuweza kuvitumia kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi. Watu huwa hawaelewi hili, huwa wanataka waelewe na kukumbuka kila wanachosoma, kitu ambacho ni sawa na kutaka kufyonza kila unachokula, haiwezekani.
Kwenye ulaji, unapokula chakula kisicho safi huwa hakikai tumboni, unakitoa kupitia kutapika na kuharisha. Kadhalika kwenye usomaji, unapoingiza maarifa na taarifa zisizo sahihi kwenye akili yako, unazirudisha kama uchafu ambao akili yako inautoa. Fikra, maneno na matendo ya hovyo yatakutoka.
Unapokula chakula kizuri kwa wingi na ulafi, unavimbiwa na hatimaye chakula kinashindwa kumeng’enywa vizuri na kufyonzwa mwilini. Kadhalika unapopata maarifa na taarifa nzuri kwa haraka bila ya kuwa na muda wa kuzitafakari kwa kina, zinaishia kukuchanganya na huwezi kuchukua hatua yoyote yenye manufaa kwako.
Kuna vyakula hovyo vya mwili (junk food) ambavyo ni vitamu kula, ila ndani yake havina virutubisho sahihi hivyo mlaji anapata utapiamlo. Kadhalika kuna maarifa yasiyo sahihi kwa akili, ambayo mtu anaweza kupenda kuyapata, lakini hayana manufaa kwake. Sukari ni chakula cha hovyo kwa mwili, udaku ni chakula cha hovyo kwa akili.
Na unapokuwa na chakula kizuri, lakini usikile kwa wakati kwa kujiambia unasubiri, chakula hicho kinaoza na huwezi tena kukila. Kadhalika kwenye maarifa na taarifa, kuna ambazo zinahitaji uchukue hatua haraka, la sivyo utakuta fursa yake imeshapita.
Kila unapopata fursa ya kujifunza kitu, chukulia kama ni chakula kipo mbele yako, hivyo jiulize kama ni chakula sahihi na kisafi, kama ndani yake kina virutubisho sahihi na chukua hatua ya kukipata chakula hicho ukijua mchango wake kwenye afya yako ya akili.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante Sana kocha. Nikweli kabisa kula chakula ni sawa na kusoma maarifa na taarifa. Muhimu ni kitu cha aina gani unaingiza. Nimelisha akili yangu chakula sahihi kupitia makala hii.
LikeLike
Ni kweli Tumaini.
LikeLike