Usiwe na mashaka juu yako, maana palipo na mashaka hapawezi kuwa na kujiamini. Haijalishi unayokabiliana nayo ni magumu kiasi gani, jiamini na jua una uwezo wa kuyashinda. Kujiamini ni nusu ya kuweza kufanya chochote. Usipojiamini, hata kitu kidogo kitakushinda.
Usijidharau, maana utawapa wengine nafasi ya kufanya hivyo na utashindwa kujisimamia kufanya makubwa. Jiheshimu wewe mwenyewe na wengine watalazimika kukuheshimu pia. Kwa kujiheshimu, utafanya yale unayopanga. Tabia ya kuahirisha mambo huwa inaanza na kutokujiheshimu mwenyewe. Na kama watu hawakuheshimu, ni kwa sababu umewafundisha wewe mwenyewe kukudharau.
Usijipe thamani ya chini, maana hivyo ndivyo wengine watakavyokuthamini pia. Jipe thamani ya juu, toa thamani kubwa na watake watu wakulipe thamani kubwa pia. Kwenye maisha hupati kile unachostahili, bali unapata kile unachopambania. Watu wapo tayari kukuthamini kwa chini iwezekanavyo, ukikubaliana nao, watakupa thamani ya chini kila wakati.
Usijiwekee viwango vya chini ili kuendana na wengine, badala yake pandisha viwango vyako zaidi na tafuta walio sahihi kwako. Wengi wanaokuzunguka, wengi unaohitaji kushirikiana nao hawataendana na viwango vyako. Hilo linaweza kukushawishi ushushe viwango vyako, lakini usifanye hivyo. Wenye viwango vya juu kama wewe wapo, pia kuna walio tayari kupandisha viwango vyao ili waweze kufanya kazi na wewe. Hivyo usishushe viwango vyako, vipandishe zaidi.
Usikubali kuwa na dharau au kiburi, hivi ni rahisi kuja pale unapoanza kupata matokeo mazuri, lakini vipinge sana, maana vitakuzuia kujifunza na kushirikiana vizuri na wengine. Kuwa mnyenyekevu na mheshimu kila mtu, hakuna utakachopoteza.
Usione haya kusema kile unachotaka kusema, kwa sababu unaona kitawaumiza wengine, kama ni ukweli, kama ndiyo kilicho muhimu, sema na fanya. Walio sahihi watakuelewa na wasio sahihi hawatakuelewa, unachotaka wewe ni walio sahihi.
Usitake kumridhisha na kumfurahisha kila mtu, hilo halitakuja kutokea, hata kama ungekuwa unafanya kitu kizuri kiasi gani. Chagua wale walio sahihi na nenda nao hao, usipoteze nguvu kukimbizana na wasio sahihi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante Sana kocha. Ninaenda kupandisha viwango vyangu
LikeLike
Vizuri Godius.
LikeLike
Asante sana Kocha.
LikeLike
Karibu Datius
LikeLike
Asante Sana kocha, napenda kupandisha viwango vyangu kwani hilo linawezekana.
LikeLike
Vizuri Tumaini.
LikeLike