Huwa tunajenga tabia, halafu tabia zinatujenga.
Tunapoanza kufanya kitu mara ya kwanza huwa ni kigumu, baadaye tukishazoea huwa tunajikuta tunafanya bila ya ugumu kabisa.
Kwenye siku yako, zaidi ya asilimia 60 ya vitu unavifanya bila ya kufikiri kabisa, unavifanya kwa mazoea kiasi kwamba unajikuta umeshafanya bila hata ya kujua.
Hivyo ndivyo siku yako inavyoisha, unajikuta umechoka kweli lakini hakuna kubwa ulilokamilisha.
Ni kwa sababu kwa sehemu kubwa, unakuwa unafanya vitu kwa tabia na mazoea kuliko mipango yako binafsi.
Kuna hali ukishajikuta upo, unajikuta umeshafanya vitu bila hata ya kufikiria. Mfano wakati upo kwenye msongo, ni rahisi kukimbilia kwenye mitandao ya kijamii, ambayo nayo inakuzidishia msongo lakini haikuachii kirahisi.
Hivyo kuondokana na tatizo hili la tabia kukupoteza, unahitaji kuanza kufanya kila kitu kwa kusudi.
Kabla hujaanza kufanya chochote, jiulize kwanza una kusudi gani kwenye kufanya kitu hicho. Usikimbilie tu kutekeleza kwa mazoea, bali jiulize kusudi lako katika kufanya kitu hicho, jiulize ni matokeo gani unategemea kuyapata kwa kile unachotaka kufanya.
Kwa njia hii, utapunguza mazoea mengi ambayo yanakupoteza, kwani kila unapoanza kitu kwa mazoea, unapojihoji utajua kama kweli hicho ndiyo sahihi kufanya au la.
Usiruhusu juhudi zako zipotee bure, kwa kila juhudi hakikisha ina kusudi, hakikisha kuna ulikoielekeza.
Usikubali muda wako ukuponyoke kama ambavyo imekuwa inatokea kwa wengi, hakikisha kila siku una vipaumbele vyako na hivyo ndiyo vikuongoze kwenye siku yako nzima.
Kabla hujafanya chochote kile, jiulize kwanza kusudi la kufanya kitu hicho na itakuwa rahisi kwako kujikamata pale unapotaka kuchepuka kwenye vipaumbele vyako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante Sana kocha, notafanya kila kitu kwa kusudi
LikeLike
Kila la kheri.
LikeLike