Kwenye maisha, lazima kuna watu utawakera, hata kama lengo lako ni kumfurahisha kila mtu, bado hutaweza kufanya hivyo.

Hivyo chochote unachofanya kwenye maisha, jua kuna watu utawakera, kuna watu watakupinga na kukataa kwa kile unachosimamia.

Lengo lako halipaswi kuwa kutokuwakera watu au kukubaliwa na kila mtu, hilo haliwezekani. Lengo lako linapaswa kuwa kuyaishi maisha yako, huku ukijua kuna watu utawakera kwa kuishi hivyo.

Ukichagua kuweka juhudi kwenye kazi zako utawakera wavivu wasiopenda kuweka juhudi na ukichagua kutokuweka juhudi utawakera wale wanajituma.

Unapokazana kumridhisha kila mtu, unaishia kutokumridhisha yeyote, unapokazana usiwakere wengi, unaishia kuwakera wengi zaidi.

Amua leo ni watu gani uko tayari kuwakera katika kuyaishi maisha yako, ili wanapokereka na kukulalamikia, unawapuuza kabisa badala ya kuumizwa na malalamiko yao.

Mimi nimeamua kuwakera wote wasiopenda kujifunza na kujaribu vitu vipya, wale wanaoona usomaji wa vitabu hauna maana, nawakera kweli kweli, kwa sababu naamini kutoka ndani ya nafsi yangu kwamba kama mtu hajifunzi, hasa kwa kusoma vitabu, basi anachagua kuwa mjinga na kujizuia kupiga hatua.

Nimeamua kuwakera wale wote wanaoamini na kutafuta njia za mkato za mafanikio, wanaoamini kuna namna ya kupata mafanikio makubwa bila kuweka kazi na muda. Kutoka ndani ya moyo wangu naamini hicho kitu hakipo, na yeyote anayekiamini najua bila ya shaka kwamba anajipotezea muda wake.

Nimeamua kuwakera wale wote wanaoamini kwenye ushirikina na imani nyingine zisizokuwa na uthibitisho, naamini kwenye sayansi na sheria za asili, ambazo zimeufanya ulimwengu kuweza kwenda mpaka sasa. Chochote kinachoenda kinyume na sheria hizo za asili, huishia kuumia. Anayeamini kwenye ushirikina na imani nyingine za aina hiyo, kama uchawi, majini, ramli na mengine, namuona ni mtu ambaye bado anaishi kwenye zama za kale.

Kuna wengi nawakera, lakini hayo makundi matatu niliyoyashirikisha hapo juu, ndiyo yenye wengi na ambayo napambana nayo kila siku.

Je wewe umechagua kuwakera watu gani? Shirikisha kwenye maoni hapo chini.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha